Tyler Thompson, aliyetambuliwa kama mmoja wa Wamarekani waliohusika katika njama ya mapinduzi iliyotibuliwa huko Kinshasa, DRC. | Picha: AFP

Katika taarifa iliyotolewa kwa Associated Press, familia hiyo iliongeza kuwa mtoto wao hajawahi kujihusisha na harakati za kisiasa.

"Tumeshtushwa na kuvunjika moyo na video tulizoona kutoka jaribio la mapinduzi," alisema mama wa kambo, Miranda Thompson, kupitia ujumbe wa X (Twitter). "Hatujuwahi kuwaza kuwa anaweza kujipata kwenye hali hii, ambayo ni kinyume kabisa na tabia yake. Tuna uhakika hakwenda Afrika kwa mipango ya harakati za kisiasa."

Thompson alikuwa miongoni mwa Wamarekani wengine wawili waliotajwa na jeshi la DR Congo kama sehemu ya jaribio lililoshindikana la kuipindua serikali ya Kinshasa alfajiri ya Jumapili chini ya kiongozi wa uhamishoni, Christian Malanga.

Wamarekani wengine wawili wanaodaiwa kuhusika walikuwa wauza bangi, Benjamin Reuben Zalman-Polun, na mtoto wa Malanga mwenye umri wa miaka 21, Marcel, ambaye alikamatwa na vikosi vya Congo.

Malanga, kiongozi anayedaiwa, alipigwa risasi na kuuawa baada ya kupinga kukamatwa, jeshi la Congo limesema. Jumla ya watu sita waliuawa katika shambulio kwenye ikulu ya rais na lingine kwenye makazi ya mshirika wa karibu wa Rais Felix Tshisekedi.

Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alilaani shambulio hilo katika mazungumzo na Tshisekedi na kutoa msaada wa uchunguzi kutoka Marekani, kulingana na muhtasari wa mazungumzo hayo.

Mama wa kambo alisema Thompson hakuwa na shughuli za kisiasa na alikuwa na hamu ya kuona dunia na marafiki wa familia. "Yeye ni mtoto mzuri, mfanyakazi hodari na kijana mwenye heshima. Hatujui kabisa jinsi alivyotumbukia kwenye shida hii," alisema.

Ubalozi wa Marekani nchini Congo ulisema Alhamisi kwamba ulikuwa bado unasubiri serikali ya Congo kutoa ushahidi kuwa watu waliokamatwa ni Wamarekani kabla ya kutoa huduma za kibalozi kwao.

Serikali ya Congo haijatoa tarehe ya watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani.

AFP