Ngoma za Burundi ni marufuku kwa wanawake kuzipiga kulingana na mila na utamaduni wao Picha: Amani Festival

Na Ramadhan Kibuga

TRT Afrika, Gitega, Burundi

Moja ya simulizi bora za nchi ya Burundi ni ngoma zake za asili. Ngoma hizi zimekuwa kivutio duniani kote kutokana na midundo ya aina yake. Mvuto na ubora wake umefanya ngoma hizi kutambulika na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Utamaduni na kuiorodhesha kama urithi wa utamaduni usioonekana.

Kiasili, ngoma hizi zilipigwa wakati wa ufalme, lakini utamaduni wake umeendelezwa hadi sasa kwenye taifa hilo la eneo la Maziwa Makuu. Na moja ya vikundi maarufu vya ngoma ni pamoja na kundi la "Abatimbo b'i Gishora" katikati mwa Burundi.

Eneo hilo la Gishora lipo karibu na mji mkuu wa kisiasa wa Gitega wenye umbali wa kilomita nane na sehemu hii inafahamika kama kitovu cha Ngoma ya Burundi na ngome kuu ya ufalme hapo zamani kuanzia karne ya 17. Na kikundi chake "Abatimbo b'i Gishora " ni maarufu sana hadi kwenye matamasha ya kimataifa.

Ukifika Gishora unawaona wanaume wa rika tofauti wakiwa miguu peku wakicheza ngoma kwenye udongo mkavu huku wakivalia sare za rangi ya bendera ya Burundi: Hao ni wapiga ngoma "Abatimbo b'igishora".

Wanazipiga ngoma huku wakiimba na kurukaruka pamoja na kulainisha viuno yao. Yote hayo kwenye mandhari nzuri ya milima iliyoinamia eneo hilo.

Ngoma za asili za Burundi zimeorodheshwa na Unesco kama urithi wa utamaduni wa dunia usioonekana. | Picha: Amani Fest

Katika eneo hili kuna nyumba za nyasi zilizozungukwa na miti ya maua kama dalili tosha ya tamaduni za jadi. Na ni moja ya kasri za zamani za kifalme.

Na hapo Gishora unakutana na ngoma mbili za kale zilizohifadhiwa vizuri.

"Ngoma hii maana yake kiimani ni kuamsha roho za wazee na kufukuza pepo wabaya."

Oscar Nshimirimana, mpiga ngoma mwandamizi aliyepata ujuzi huo kutoka kwa babu yake

Mkuu wa kikundi cha wapiga ngoma au Abatimbo b'i Gishora Oscar Nshimirimana alieleza TRT Afrika siri ya ngoma hizo, " Ngoma hizi zilianza wakati wa ufalme. Zilikuwa zinapigwa katika sikukuu rasmi kama sikukuu ya nafaka maarufu, "Umuganuro."

''Ngoma mbili hasa, Ruciteme na Murimirwa zimedumu kwa zaidi ya miaka 118. Na ninaweza kusema bila kusita kwamba ngoma hizi ndio chanzo cha kupatikana ngoma nyingine katika nchi nzima ya Burundi,'' aliendelea kusema.

Kawaida, ngoma hii ya Burundi asili yake ni mchanganyiko wa midundo, mchezo, mashairi na nyimbo za kitamaduni. "Tunapiga ngoma hii kwa vile ndio burudani yetu. Hii iko kwenye damu," amesema Mathias Niyonkuru baada ya kuburudisha watu huku bado anatiririka jasho katika uso wake.

Kwa upande wake, Oscar Nshimirimana, mpiga ngoma mwandamizi yeye alipokea usia kutoka kwa babu zake. Ameambia TRT Afrika kuwa: "Ngoma hii maana yake kiimani ni kuamsha roho za wazee na kufukuza pepo wabaya."

Kiasili pia ngoma hizi zilipigwa wakati wa sherehe maalumu kama vile kuzaliwa kwa mtoto, mazishi na kutawazwa kwa mfalme na kadhalika.

"Ngoma hizi zilianza wakati wa ufalme. Zilikuwa zinapigwa katika sikukuu rasmi kama sikukuu ya nafaka maarufu "Umuganuro."

Mkuu wa kikundi cha wapiga ngoma au Abatimbo b'i Gishora Oscar Nshimirimana

Mwendelezo wa kizazi kimoja hadi kingine

Ngoma ya Burundi imejenga utamaduni wa urithi kwa jamii. Mpiga ngoma Butoyi Jean anasema, "Sio baba yangu pekee aliyekuwa mpiga ngoma, lakini pia mababu zetu, yaani ni kizazi kinarithiwa, kwa maana hiyo kwangu ngoma ni mwendelezo wa ukoo."

Kiutawala ngoma za Burundi ni ishara ya mamlaka kuanzia ufalme hadi wakati huu wa Jamuhuri.

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye ambae ana asili ya eneo hili la Gitega na yeye mara kwa mara huburudika katika matamasha ya kijijini kwa kuongoza mdundiko wa ngoma na hivyo kuleta hamasa kwa wananchi kuchangamkia burudani hiyo.

Lakini ukitaka kujua undani zaidi, ngoma hizi zimegawanyika kwenye mdundo na sauti na zikiwa na majina na kazi maalumu. Steve Nkurunziza mpiga ngoma kwa zaidi ya miaka 20 anasema, "Hii ngoma ya katikati inaitwa' Inkiranya'. Ni ngoma kubwa iliyochapishwa bendera ya taifa. Shughuli yake muhimu ni kuchanganya midundo ya ngoma zote. Inaonyesha pia ishara zote ikiwa ni pamoja na kuanza, kugeuza mtindo na kumaliza.

"Hizi nyingine za upande wa kulia zinaitwa, ' Ibishikizo' Kazi yake ni kuleta "base" kwenye ngoma. Hata uwe wapi unasikia inavyodunda"

''Hizi nazo za upande wa kushoto zinaitwa "Amashako." Ngoma hizi zinaleta "solo" katika mdundo, aina nyingine kabisa ya sauti"

Steve Nkurunziza akifafanua baadhi ya nafasi za wapiga ngoma anaeleza kwamba "Kuna baadhi ya wapinga ngoma wanashikilia mtindo mmoja kwenye mchezo lengo lake ili kubaki na "rhythm ya ngoma."

Kisha akisititiza ukitizama kwenye ngoma yetu utaona wapigaji tunakuja kwenye kuburidisha na ngoma kubwa ya kati huku tukiweka fimbo shingoni. "Maanake ni nini?" Ni ishara kuwa hapa tunakula kiapo na kuapa kwa kusititiza kwamba hatuwezi kuisaliti nchi yetu. Hivi ndivyo ilivyokuwa wakati wa mfalme."

Ngoma hizi zimekuwa kivutio kote duniani kutokana na midundo yake yenye mvuto na tayari zimeshirikishwa katika filamu maarufu na albamu kadhaa kote ulimwenguni.

Serikali imeweka masharti ya kutopiga ngoma hizi bila ruhusa ili kuhifadhi hadhi yake| Picha: Amani Fest

Inatambulika kimataifa

Kutokana na ubora wake, tangu mwaka wa 2014, ngoma hii ya Burundi inatambulika sasa kimataifa. Hii ni baada ya Shirika la Umoja Mataifa la Utamaduni UNESCO kuiorodhesha ngoma hii kama urithi wa utamaduni usioonekana.

Na ili kuupa nguvu utamaduni huu ,Serikali ya Burundi imepiga marufuku ngoma hizi kupigwa bila idhini ili kulinda mila zinazoendana na ngoma za taifa hili. Moja wapo ni mwiko kwa mwanamke yoyote kuzipiga kama ilivyokuwa wakati wa ufalme ikidaiwa kwamba ngoma kwenye muundo wake ina "viungo na maumbile" ya mwanamke.

Aidha Serikali ya Burundi imepiga marufuku upigaji wa ngoma katika mikutano isiokuwa rasmi ikiwemo sherehe za kitamaduni na harusi katika jaribio la kuhifadhi mila hiyo ya zamani ambayo sasa inajulikana kimataifa.

Na tangu mwaka wa 2017 serikali iliazimia pia uwepo wa ada za kulipia upigaji wa ngoma kwenye sherehe mbalimbali ikiwa ni franka za Burundi laki tano sawa na dola 165.

TRT Afrika