Nyashinski alikuwa anatarajiwa kushiriki katika Tamasha ya Madaraka pamoja na waimbaji wengine. / Picha: Nyashinski

Na Charles Mgbolu

Nyota wa muziki nchini Kenya Nyamari Ongegu, anayejulikana na mashabiki kama Nyashinski, amejiondoa kwenye tamasha lijalo la USA Madaraka Festival 2024 baada ya timu kushindwa kupata viza ya Marekani.

Katika ujumbe wake uliotumwa kwenye mitandao ya kijamii, Nyashinski, ambaye alishinda Tuzo za Afrika Mashariki za Acts Entertainment Awards mwaka wa 2022, alisema hatoshiriki licha ya juhudi za waandaaji wa tamasha hilo kutafuta viza ya timu yake kuingia Marekani.

"Tulitarajia sana ziara hiyo, na tunaomba radhi kwa usumbufu wote ambao umesababishwa," taarifa kutoka Nyashinski ilisema.

Madaraka Festival ni tamasha la muziki wa Kiafrika, utamaduni, na jamii linaloandaliwa katika miji yote nchini Marekani.

Toleo la 2024, ambalo ni la 10, limeratibiwa kuanza Dallas mnamo Mei 25 na kufanya fainali kubwa huko Seattle mnamo Juni 17 na 18.

Kulingana na waandaaji, Nyashinski anaongoza hafla hiyo na mwimbaji wa Uganda Eddy Kenzo na mwimbaji wa Cameroon Naomi Achu.

Wengine ni msanii wa reggae-dancehall wa Sudan Kusini Dynamq na mwimbaji na mpiga ngoma wa kundi la Sauti Sol ya Kenya - Savara.

Haijulikani kwa wakati huu ikiwa wasanii wengine wanaotarajiwa kutumbuiza wamepata viza vya kusafiri.

''Hasara kwao''

Katika majibu yao, mashabiki wameukosoa ubalozi wa Marekani nchini Kenya kwa kushindwa kutoa viza kwa Nyashinski na timu yake.

‘’Kuwa nchi ya kimaskini kutatuathiri daima, bila kujali tunafanya nini. Hata hivyo, hasara ni yao,’’ aliandika shabiki, Roman Bomu, kwenye Instagram.

Nyashinski hajawahi kuwa na shida siku za nyuma kuhusu kusafiri kwenda Marekani; ametumbuiza katika miji kadhaa na ameishi huko kwa miaka 10 wakati wa mapumziko.

Alirejea Kenya mwaka 2016 ili kuendelea na harakati zake za muziki.

Safu ndefu wa watu kunyimwa viza

Wasanii wa Kiafrika mara nyingi wamekuwa na ugumu wa kupata viza vya kutumbuiza katika nchi za Ulaya, bila sababu za wazi zinazotolewa za kunyimwa.

Hii mara nyingi imesababisha makasiriko ya wasanii mtandaoni.

Mnamo Januari 2023, Emma Nzioka, mwigizaji wa Kenya na DJ anayejulikana kama Coco Em, alipaswa kufanya show Cape Verde na alilipangiwa kusafiri kupitia Uholanzi.

Coco Em amezungumzia kuhusu ugumu wa wasanii wa Kiafrika kupata viza za kusafiri Ulaya. / Picha: Coco Em

Lakini Coco alinyimwa viza ya usafiri, na kusababisha taharuki kutoka kwa mashabiki wake mtandaoni.

Msanii mwengine wa Kiafrika, nyota wa Afropop Yemi Alade kutoka Nigeria, alinyimwa viza ya Schengen mnamo Januari 2023.

Mnamo 2022, Alade pia alinyimwa viza ya Canada kwa tamasha la International Africa Nights.

Mnamo 2019, wasanii wawili wa Kitanzania, DJ Duke na MCZO, walinyimwa viza ya kwenda Marekani.

Mashabiki wamekashifu vitendo hivi na kuvitaja kuwa ni "kudharauliwa kabisa kwa wasanii wa Kiafrika."

TRT Afrika