Rais William Ruto atafanya ziara rasmi Marekani kutoka 20 hadi 24 Mei 2024/ Picha Ikulu Kenya  

Rais William Ruto anaanza ziara yake rasmi nchini Marekani inayofanyika kati ya Mei 20 hadi 24, 2024.

Mara ya mwisho kwa Kenya kufanya ziara kama hii nchini Marekani ilikuwa ni miongo miwili iliyopita. Hii pia ni ziara ya kwanza rasmi ya rais wa Afrika tangu 2008.

Atakutana na Rais Joe Biden 23 Mei, 2024.

Rais Ruto atafanya mikutano mikuu ya nchi mbili na Rais Biden kuangazia zaidi Kenya kiuchumi, afya na ushirikiano wa usalama wa Marekani na kujadili maendeleo ya kikanda katika bara.

Mbali na kujadili masuala ya mahusiano wa kisiasa na uchumi kati ya Kenya na Marekani , Ikulu ya Kenya inasema Rais Ruto pia atatembelea studio za msanii wa kimataifa anayetengeneza filamu, Tyler Perry .

Ikulu imedai kuwa rais ataenda huko kutafuta nafasi za ushirikiano na mwanasanaa huyo ili kuongeza nafasi za kazi.

"Rais Joe Biden anatumai mazungumzo hayo yanaonyesha kwamba Marekani bado imewekeza barani Afrika katika kipindi cha ushindani unaokua na wapinzani wake wakuu wa kijiografia, China na Urusi. Beijing na Moscow zimeshirikiana kwa ukali na washirika katika bara katika miongo miwili iliyopita," wataalam wa siasa kutoka shirika la Crisis group wanasema.

Ziara ya rais Ruto inafuatia mualiko kutoka kwa Rais Biden.

"Pia inaonyesha umuhimu wa kimkakati wa Kenya kwa Marekani kama nanga inayoongoza katika kanda na lango kuu la kibiashara kwa Afrika Mashariki," Msemaji wa rais wa Kenya Hussein Mohammed alisema.

TRT Afrika