Roger Whittaker ambae wazazi wake ni raia wa Uingereza alizaliwa katika Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi/ Picha : Others

Mwimbaji na mtunzi wa nyimbo za asili wa Uingereza Roger Whittaker amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 87.

"Maisha yake, usanii na urithi wake umekuwa wa maana sana kwa wengi duniani kote. Tunashukuru kwamba zawadi ya muziki wake inabaki kwetu," rafiki yake Jesse Wagoner alisema wakati akitangaza kifo hicho siku ya Jumatatu.

Taarifa ya familia imesema mwimbaji huyo alifariki Septemba 13 katika hospitali moja kusini mwa Ufaransa ambako alikuwa anaishi baada ya kustaafu.

Whittaker ambae wazazi wake walikuwa Waingereza alizaliwa katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Anasifika katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa utunzi wake wa mwaka 1982 ‘My Land is Kenya,’ uliosherehekea uzuri na fahari ya nchi yake ya kuzaliwa.

My land is Kenya, so warm and wild and free

You'll always stay with me here in my heart

My land is Kenya, right from your highlands to the sea

You'll always stay with me here in my heart, here in my heart

Hapo awali alizungumzia jinsi muziki wa Afrika Mashariki ulivyoacha alama katika utoto wake.

"Katika zaidi ya miaka 30 ya kuimba na kucheza sauti za muziki - upigaji wa ajabu, na midundo hiyo ya ajabu, ya kuambukiza - imechukua sehemu kubwa katika kila kitu ambacho nimewahi kuandika na kuimba."

Katika kuomboleza, Waziri Mkuu wa Baraza la Mawaziri wa Kenya Musalia Mudavadi alisema, "Muziki wa kutuliza wa Whittaker uligusa mioyo ya mamilioni ulimwenguni."

"'My land is Kenya ' ilichangia pakubwa katika kuitangaza Kenya kama kivutio cha kuvutia cha watalii," alisema.

"Apumzike kwa Amani, aliandika muziki mzuri wenye maneno ya dhati," alisema aliyekuwa katibu mkuu wa masuala ya kigeni Macharia Kamau.

TRT Afrika na mashirika ya habari