Mbali na maeneo yenye migogoro, haki za watoto pia ziko hatarini, hasa kutokana na magonjwa na umaskini.

Na Fathiya Bayusuf

TRT Afrika, Mombasa, Kenya

Hakuna wakati muhimu kuwa mzazi kama sasa. Kila unapotazama inaonekana kuhujumu ulezi wa watoto kwa namna moja au nyingine.

Vita visivyokuwa na maana, usajili wa watoto katika makundi ya wapiganaji, ukatili, visa vya unyanyasaji wa watoto, mashambulio katika mitandao ya kijamii, magonjwa, dawa za kulevya au hata mabadiliko ya tabia nchi.

Kila kitu kinaonekana kuwa silaha ya maangamizi kwa watoto.

Hii inaonesha umuhimu wa azimio la kimataifa la kuhifadhi haki za watoto. Na hakuna azimio la Umoj awa Mataifa lililoungwa mkono na serikali nyingi zaidi kuliko hii ya haki za watoto ya 1989.

"Umoja wa Mataifa umethibitisha zaidi ya ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto 315,000 katika maeneo yenye migogoro kati ya 2005 na 2022,'' anasema Catherine Russell, Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, na kuongeza, "Na haya ni matukio pekee ambayo yamethibitishwa ambayo ina maana kwamba idadi halisi ya ukiukaji bila shaka ni kubwa zaidi.''

Zaidi ya maeneo yenye migogoro, haki za watoto pia ziko hatarini, hasa kutokana na magonjwa na umaskini.

Katika eneo la Likoni, Mombasa, Pwani ya Kenya, kituo cha watoto yatima cha Jannatul Firdaus kinafungua ukurasa wa matumaini. Rashid Kishki, mwenye umri wa miaka 12, aliwasili kituoni hapo miaka mitano iliyopita akiwa na umri wa miaka nane, akiwa na ndoto za kuwa na wazazi wake wa asili.

"Ni changamoto kubwa kuwa hapa. Nashukuru kwa mapokezi mazuri, lakini moyoni mwangu, bado nataka kujua jinsi ilivyo kuwa na wazazi, kuhisi upendo wa mama na baba,” anasema Rashid, mtoto yatima anaelelewa katika kituo hicho.

Rashid, mwanafunzi wa darasa la sita, anakabiliana na upweke na uhitaji wa mahitaji muhimu. Anaelezea jinsi chakula mara nyingine kinavyokuwa kidogo, mavazi yanavyokosekana, na msongamano wa watoto kutoka na uhaba wa vyumba vya kutosha.

"Tunahitaji msaada zaidi, chakula cha kutosha, mavazi safi, na mahali pazuri pa kulala. Nyakati nyengine, nahisi upweke, hata kama napenda kuwa hapa," anasema Rashid, mtoto yatima.

Nae Khadija Anton, msichana mwenye umri wa miaka 18, anaishi na ulemavu wa miguu na anatamani kuhisi mapenzi ya wazazi. Alikuja kituoni akiwa mdogo baada ya kufiliwa na wazazi.

Kauli mbiu ya Siku ya Watoto Duniani 2023 ni 'Kila mtoto, Kila haki' /Picha : TRT Afrika 

"Nahitaji miguu bandia na mashine ya kushonea ili niweze kujimudu kimaisha,'' anaambia TRT Afrika.

Anaelezea changamoto ya kukosa wazazi na jinsi maisha kituoni yanavyokuwa tofauti na kuwa na familia.

"Changamoto nyingine ni kukosa wazazi. Ningependa kuwa nao, wanipatie mapenzi yao na kusimamia mahitaji yangu. Nahuzunika sana, na maisha hapa kituoni ni tofauti kabisa na kuwa na wazazi," anasema Khadija.

Kwa mujibu wa Shirika la Watoto Duniani UNICEF watoto milioni 400 - au takriban mtoto 1 kati ya 5 - wanaishi au wanakimbia maeneo yenye migogoro.

''Wengi wao wamehamishwa mara kadhaa, wakihatarisha kutengwa na familia zao, kupoteza miaka muhimu ya elimu, na kuvunja uhusiano na jamii zao,'' anasema Catherine Russell wa UNICEF.

"Changamoto nyingine ni kukosa wazazi. Ningependa kuwa nao, wanipatie mapenzi yao na kusimamia mahitaji yangu. Nahuzunika sana, na maisha hapa kituoni ni tofauti kabisa na kuwa na wazazi."

Khadija Anton, mwanafunzi kutoka Kituo cha Watoto Yatima, Mombasa, Kenya.

Kituo cha Jannatul Firdaus, Mombasa, chenye zaidi ya watoto 80, kimekuwa nyumba ya watoto hawa kwa miaka mingi, kikitoa mahitaji muhimu na elimu ya dini.

Mama Dhahabu Mwalimu, mlezi wa kituo, anatambua changamoto za kuwalea watoto hao na kusisitiza umuhimu wa kuwapa upendo, usalama, na malezi bora. Ingawa rasilimali ni haba, anajitahidi kutoa yote anayoweza.

"Kuwalea hawa watoto si jambo rahisi. Wanahitaji mahitaji yao kutimizwa, lakini mara nyingine, rasilimali zinakuwa ni finyu,'' anasema mama Dhahabu. ''Wanapokuwa wachanga, inaweza kuwa vigumu kununua vitu wanavyohitaji, na wakati mwingine hata chakula kinaweza kuwa changamoto. Tunashukuru kwa wasamaria wema wanaotusaidia," anaongezea.

Kwa upande mwengine, wanasaikolojia wanasisitiza umuhimu wa watoto kupokea upendo na msaada wa kisaikolojia.

Lucy Mjomba, mshauri nasaha kutoka Mombasa, anasema, "Kwa kuwaonyesha upendo, tunaweza kusaidia watoto hawa kubadilisha mtazamo wao. Wanapofika kituoni na kupata mazingira yanayowasaidia kubadilisha maoni yao, wanaweza kudhibiti hali yao ya kihisia na kujenga mustakabali bora."

Wakati wa kusherehekea Siku ya Watoto Duniani, watoto hawa wanathibitisha ujasiri wao na azma yao ya kusonga mbele, wakiwa na imani kwamba wanaweza kujenga familia mpya na kufanikiwa.

Na kwa kufuata kauli mbiu ya mwaka 2023 ya Siku ya Watoto Duniani, 'Kila mtoto. Kila haki,' shinikizo linaongezwa kote duniani kuwapa watoto wote haki zao kamili.

TRT Afrika