Vita vimepamba moto kati ya vikosi vya jeshi la Sudan na Vikosi vya RSF, tangu Aprili 2023/ Picha: Wengine

Katika jimbo la mashariki la Al-Jazirah, Kamati ya Upinzani ya Jiji la Rufaa, kikundi cha watu wa kujitolea kusaidia wahasiriwa wa vita, ilitangaza kuwa raia 25 waliuawa na idadi isiyojulikana kujeruhiwa katika mashambulizi ya RSF.

Katika taarifa yake, kamati hiyo ilisema kuwa majeruhi hao walitokea kufuatia shambulio la vikosi vya RSF kwenye miji ya Rufaa na Tamboul pamoja na vijiji kadhaa mashariki mwa Al-Jazira, ambapo nyumba zilivamiwa.

Hakuna upande wowote katika mzozo huo ambao umejibu madai kuhusu mauaji ya raia.

Imran Abdullah, mjumbe wa ofisi ya ushauri ya kamanda wa RSF, alisema katika chapisho kwenye X kwamba vikosi vyao vimechukua udhibiti wa mji wa Tamboul.

Jeshi la Sudan halijazungumzia madai hayo.

Matukio ya Al-Jazira yanakuja siku mbili baada ya Abu Aqla Muhammad Ahmed Kikil, kamanda wa RSF katika jimbo hilo, kutangaza kuhama na vikosi vyake kwa jeshi la Sudan.

Vita nchini Sudan vinazidi kupamba moto, huku vikihusisha Jeshi la Sudan dhidi ya RSF tangu kuibuka kwa mgogoro wa kisiasa Aprili 2023.

Vikosi hivyo viwili viko katika mapigano makali ya kuwania eneo la Al-Jazira, ambalo liko chini ya udhibiti wa wanajeshi tangu mwishoni mwa mwaka jana.

Pande zote mbili zimeshutumiwa kwa uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na kuwalenga raia, kupiga makombora kiholela katika maeneo ya makazi, kuzuia usambazaji wa misaada pamoja na kuipora.

TRT Afrika