Tanzania inashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na idadi kubwa ya Simba kuliko nchi yoyote barani Afrika, sababu inayoifanya nchi hiyo kuwa na zaidi ya asilimia 70 ya idadi ya Simba barani Afrika./Picha: Getty

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Kwa muda mrefu sasa, Tanzania imejizoelea umaarufu kama ardhi ya Mlima Kilimanjaro na hifadhi nzuri na kipekee ya Serengeti.

Sababu hizo kuu mbili na nyinginezo nyingi, zimekuwa zikiwavutia mamilioni ya watalii kila mwaka kuitembelea nchi hii inayopatikana katika katika ukanda wa Afrika Mashariki kwenda kushuhudia utajiri wake wa maliasili.

Hata hivyo, kwa sasa, utasamehewa ukiita Tanzania kuwa Paradiso ya Simba Duniani, kufuatia utafiti uliofanywa hivi karibuni.

Tanzania inashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na idadi kubwa ya Simba kuliko nchi nyingine yoyote barani Afrika, na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa na zaidi ya asilimia 70 ya idadi ya Simba barani Afrika.

Kwa mujibu wa utafiti uliotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Aprili 22, Tanzania ina jumla ya Simba 17,000, ikifuatiwa na Afrika Kusini yenye Simba 3,284, wakati Botswana inashika nafasi ya tatu ikiwa na Simba 3,064.

Tanzania inashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na idadi kubwa ya Simba kuliko nchi yoyote barani Afrika, sababu inayoifanya nchi hiyo kuwa na zaidi ya asilimia 70 ya idadi ya Simba barani Afrika./Picha: Getty

Kenya iko katika nafasi ya nne ikiwa na jumla ya Simba 2,515, wakati Zambia inashika nafasi ya tano kwa kuwa na wafalme wa nyika wapatao 2,349.

Utafiti huo uliangazia mifumo ya ikilojia ya Nyerere-Selous-Mikumi, Saadani-Wami Mbiki na Serengeti, ya nchini Tanzania.

Sensa hiyo ya wanyamapori pia ilibaini uwepo wa chui 24,000 katika mifumo hiyo ya ikolojia.

Si jambo la kushangaza

Dr Maurus Msuha, kutoka mradi wa SOKNOT unaoratibiwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) anasema si ajabu kwa Tanzania kuendelea kuongoza kwa idadi kubwa ya Simba na wanyamapori wengine kutokana na sera, sheria na ujenzi wa taasisi imara za kusimamia hifadhi zinazotekelezwa nchini Tanzania.

“Masuala ya uhifadhi yana mchango mkubwa sana katika maendeleo ya utalii, na ndio maana maeneo mengi nchini Tanzania yametengwa kwa ajili ya hufadhi,” anaimbia TRT Afrika katika mahojiano maalum.

Mtaalamu huyo wa masuala ya wanyamapori anasema kuwa mipango ya uhifadhi nchini Tanzania imechangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa idadi kubwa ya wanyamapori.

Utafiti huo uliangazia mifumo ya ikilojia ya Nyerere-Selous-Mikumi, Saadani-Wami Mbiki na Serengeti, ya nchini Tanzania./Picha: Getty

Tanzania ina jumla za hifadhi za taifa 22, zinazosimamiwa na TANAPA.

Kulingana na Dr Msuha, kinachoipa Tanzania nafasi ya kuwa na wanyamapori wengi zaidi barani Afrika ni uwepo wa wanyama hao katika maeneo yaliyohifadhiwa.

“Tanzania ndiyo nchi pekee yenye muunganiko wa aina sita za uoto wa asili ambazo ni sababu tosha ya kuipa uwezo wa kuwa na aina nyingi za wanyamapori,” anaelezea.

Dr Msuha anaongeza kuwa Tanzania imetenga maeneo ya uhifadhi yenye kutoa nafasi ya kuongeza idadi ya Simba katika mfumo wa ikolojia ya Serengeti, unaohusisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, mapori ya akiba ya Maswa, Kijereshi, Pololeti, Grumeti na Ikorongo.

Sio Simba tu

Tanzania ina jumla ya nyati 225,000, ikifuatiwa na Afrika Kusini yenye mbogo 46,000./Picha: Getty

Utafiti huo, ambao umefanywa kwa ushirikiano na mashirika mengine ya uhafadhi nchini Tanzania, kama vile TAWIRI, TANAPA, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Shirika la Hifadhi la Frankfurt na Chuo Kikuu cha Glasgow, unaonesha kuwa Tanzania ina jumla ya nyati 225,000, ikifuatiwa na Afrika Kusini yenye nyati 46,000.

Kenya inashika nafasi ya tatu ikiwa na nyati 42,000 wakati Zambia ina wanyama hao wapatao 41,000.

Utafiti uliofanywa kati ya Novemba 2022 na Machi 2023, ulibaini uwepo wa tembo 60,000 nchini Tanzania, na hivyo kuifanya kuwa nchi ya tatu kuwa na idadi kubwa ya wanyama hao wakubwa duniani.

Botswana inashika nafasi ya kwanza ikiwa na tembo 130,000, ikifuatiwa na Zimbabwe yenye tembo 100,000.

Athari za shughuli za kibinadamu

Licha ya utafiti huo kubaini uwepo wa nyumbu milioni 1.6 katika ikolojia ya Serengeti, kumekuwepo na upungufu mkubwa wa twiga, kudu wakubwa na puku, ambao walikuwa 1,679, 1,414 na 496, mtawalia.

“Shughuli za kibanadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa kama vile kilimo, ujenzi na ufugaji ni tishio kwa ustawi wa wanyamapori hususani katika ikilojia ya Nyerere-Selous-Mikumi,” anaonya Dk Eblate Mjingo, Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI.

Tanzania imelenga kupokea watalii milioni 5, ifikapo mwaka 2025./Picha: Getty

Maendelo ya Utalii

Serikali ya Tanzania imenuia kuchangia shilingi bilioni 4 za Kitanzania (dola milioni 1.5) kutoka katika mfuko wa maendeleo ya utalii ili kufanikisha sensa ijayo ya wanyamapori ambayo pia itajumuisha wanyama wengine kama vile viboko na mamba.

Zaidi ya watalii milioni 1.8 walitembelea Tanzania mwaka jana, kutoka milioni 1.3 waliofika nchini humo mwaka 2022, na kuiingizia nchi hiyo dola milioni 3.4.

Tanzania imelenga kupokea watalii milioni 5, ifikapo mwaka 2025.

TRT Afrika