Sehemu ya kiwanda cha Sukari cha Mtibwa kilichopo wilayani Turiani, mkoani Morogoro nchini Tanzania./Picha: Wengine

Watu 11 wamepoteza maisha na wengine wawili kujeruhiwa kufuatia mlipuko uliotokea katika kiwanda cha kuzalisha sukari nchini Tanzania.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo, vimemnukuu kamanda wa Zimamoto na Uokoaji mkoani Morogoro, Shaban Marugujo ambaye amesema tukio hilo limetokea Mei 23, 2024 kufuatia kulipuka kwa mtambo wa mfumo wa joto la kuzalishia sukari ndani ya kiwanda cha Mtibwa, kilichopo Morogoro, nchini Tanzania.

Kulingana na Marugujo, mlipuko huo ulitokea wakati wafanyakazi wa kiwanda hicho wakijiandaa na uzalishaji wa bidhaa hiyo.

"Ni kweli kuwa tukio la namna hiyo limetokea ndani ya kiwanda cha Mtibwa, na ni jambo la kawaida kuwepo na joto la kiwango fulani ili sukari iweze kuzalishwa," ameeleza.

Marugujo ameongeza kuwa timu ya waataalamu imepiga kambi katika kiwanda hicho ili ili kuweza kubaini chanzo halisi cha kutokea kwa mlipuko huo.

TRT Afrika