Wakili Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dkt Boniface Luhende./Picha: Wengine  

Tanzania imeokoa zaidi ya dola milioni 575 ( trilioni 1.5) baada ya kushinda mashauri 15 ya usuluhishi kati ya 19 yaliyokuwa yamefunguliwa ndani na nje ya nchi.

Mashauri hayo yalifunguliwa kati ya Julai 2023 na Aprili 2024.

Kulingana na Wakili Mkuu wa serikali ya Tanzania Dk Boniphace Luhende, mashauri ya madai 762 kati ya 7, 813 yaliyoendeshwa na ofisi yake, yamekamilika.

"Pia ofisi hii imeshughulikia notisi za miezi mitatu zipatazo 723 zilizowasilishwa katika kipindi cha Julai 2023 hadi Aprili 2024, ambapo kwa asilimia kubwa, notisi hizo zilihusu masuala ya ardhi, kazi na mikataba," alielezea Wakili huyo Mkuu wa Tanzania, jijini Arusha, Tanzania, Mei 21, 2024.

Kulingana na Dk Luhende, Tanzania imeendesha na kushinda mashauri tofauti likiwemo la ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda mpaka Chongoleani-Tanga ambapo.

“Iwapo serikali ingeshindwa shauri hili, mradi huu unaoghraimu dola bilioni 3 (trilioni 8) usingeweza kutekelezwa,” ameongeza.

Wakati huo huo, Tanzania imewataka mawakili wa serikali kutoa ushauri mapema kabla mambo hayajaharibika.

Nchi hiyo pia imesisitiza umuhimu wa mawakili hao kutoa ushauri mapema pale wanapoona dalili ya mambo kuharibika, ili kuepusha migogoro mbali mbali.

TRT Afrika