Ronald Sonyo na Fathiya Bayusuf
Wageni mbalimbali wakiongozwa na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaaliwa wamejitokeza mapema hii leo kuadhimisha Sherehe za Baraza la Maulid ambazo kitaifa zimefanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, katika mji mkuu wa Tanzania Dodoma.

Maadhimisho hayo pia, yamehudhuriwa na viongozi wa dini nyengine kutoka madhehebu ya dini ya kikristo ikiwemo Baraza la Maaskofu wa Kikatoliki Tanzania-TEC pamoja na Jumuia ya Kikristo Tanzania CCT.
"Tunashukuru kwa kushirikiana na ndugu zetu waislamu na kuenda kusimama kama taifa moja na tunafurahi," amesema Mchungaji Moses Matonya.
Shamrashamra hizo mara nyingi huendelea kwa muda wa mwezi mzima katika maeneo tofauti duniani.

Waandaji wamesema sherehe hizi za maulid ni za kimkakati kijamii na kiimani huku kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Maulid na maendeleo.
Wakati wa hotuba yake kwa Baraza hilo Waziri Mkuu wa Tanzania Kasim Majaaliwa alionya kuhusu hatari inayoweza kuwapata vijana wanaojiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya.
"Niwasihi viongozi wetu kuendelea kuisaidia Serikali kupiga vita madawa ya kulevya kwa vijana kwa sababu sauti yenu inasikika kwa haraka na jamii."
"Niwasihi viongozi wetu kuendelea kuisaidia Serikali kupiga vita madawa ya kulevya kwa vijana kwa sababu sauti yenu inasikika kwa haraka na jamii," amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Utunzaji wa maadili na kuvunjika kwa ndoa ni miongoni mwa mada zilizotawala katika sherehe za Maulid ya mwaka huu.
Kwengineko nchini Kenya, waumini wa dini ya Kiislamu kutoka Pwani ya nchi hiyo, Mombasa, kama sehemu ya maadhimisho hayo, kihistoria hufanya msafara wa amani unaojumuisha mamia ya wakazi wa mji huo, ambao wanatoka viunga tofauti vya mji na hatimae kukusanyika katika uwanja maarufu wa Makadara.

Washiriki wa msafara huo ni pamoja na wanafunzi kutoka madrasa tofauti na taasisi za Kiislamu ambapo huimba nyimbo za nasheed zenye lengo la kumsifu Mtume Muhammad (Rehema na Amani Ziwe Juu Yake) huku rangi za kijani na nyeupe zikitawala.
Katika maadhimisho hayo, ni desturi kwa watoto kuvalishwa kanzu na mavazi ya kuvutia, taswira ambayo huvutia wakazi wengi ambao hujitokeza pembezoni mwa barabara kuangalia msafara huo.

Waislamu huadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad, au Milad un Nabi kama inavyojulikana katika dini ya Kiislamu. Siku hiyo huadhimishwa kila siku ya tarehe 12 ya Rabi’ al-Awwal ambao ni mwezi wa tatu wa kalenda ya Kiislamu.