Waziri, Mary Goretti Kitutu na kakake walifikishwa mbele ya Mahakama ya kupambana na ufisadi siku ya Alhamisi | Picha kutoka Anti-Corruption Unit Uganda 

Waziri katika serikali ya Uganda amewekwa rumande akishitakiwa kwa madai ya ufisadi. Inadaiwa alichukua mabati yaliyokusudiwa kuwasaidia watu wanaoishi katika eneo la Kaskazini mwa nchi, eneo la Karamoja .

Kitengo cha kupambana na ufisadi nchini Uganda kinasema mashtaka dhidi ya ndugu hao ni pamoja na ''njama ya kulaghai na kupoteza mali ya umma baada ya kudaiwa kugeuza mabati yaliyokusudiwa kwa jamii zilizo hatarini katika eneo dogo la Karamoja.''

Taarifa kutoka kwa shirika la kupambana na ufisadi iliongezea kuwa wamerudishwa rumande hadi Aprili 12, 2023.

Waziri Mary Goretti Kitutu na kaka yake walifikishwa mbele ya Mahakama ya Kupambana na Ufisadi siku ya Alhamisi. Bado hawajawasilisha ombi lao.

Mabati hayo yalitengwa kwa ajili ya makazi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu huko Karamoja, eneo ambalo lina maendeleo kidogo hasa kwa sababu ya changamoto ya kutokuwa na usalama . Karamoja iko Kaskazini Mashariki mwa Uganda na inapakana na Kenya na Sudan Kusini.

Kitutu ndiye waziri anayehusika na maendeleo ya Karamoja.

Kashfa hiyo ilisababisha malalamiko makubwa ya umma katika nchi hiyo ambapo ufisadi wa serikali umeenea. Ni nadra kwa afisa mwenye nafasi kubwa kama ya Kitutu kushtakiwa kwa ufisadi, na yeye ndiye mhusika mkubwa zaidi serikalini kufikishwa katika mahakama ya ufisadi kwa miaka mingi.

AFP