Nyota huyo wa zamani wa Hispania allichaguliwa kuingoza Barcelona mwezi Novemba, 2021./Picha: AP 

Xavi atasalia kama Kocha wa Barcelona, licha ya awali kutangaza kuwa angeachana na klabu hiyo mwisho wa msimu huu, miamba hao wa Ligi Kuu ya Hispania wameiambia AFP siku ya Jumatano.

Vyombo vya habari vya Hispania vimeripoti kuwa Xavi, mwenye umri wa miaka 44, alibadili maamuzi yake kufuatia kikao cha pamoja na Rais wa Klabu hiyo Joan Laporta na mkurugenzi wa michezo, Deco.

Uamuzi wa nyota huyo wa zamani wa Hispania unakuja wiki moja baada ya Barcelona kutolewa na PSG katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mabingwa hao watetezi wapo nyuma kwa alama 11 dhidi ya Real Madrid, baada ya kupoteza mchezo dhidi yao siku ya Jumapili, Aprili 21.

'Ukombozi'

Kiungo huyo fundi wa zamani wa Barcelona alisema kuwa alijisika kukombolewa baada ya kufikia uamuzi wake wa kuachia ngazi kuifundisha klabu hiyo.

Mara kadhaa, alikaririwa akisema kuwa hiyo ilikuwa ni 'ndoto' yake kuifundisha Barcelona, na baadaye kukiri kuwa alizidiwa na shinikizo linalotokana na kuifundisha klabu hiyo.

"Inakufanya ujisikie kuwa wewe si chochote," alisema baada ya kichapo cha nyumbani cha 5-3 kutoka kwa Villarreal.

"Ilitokea kwa makocha wote: Pep (Guardiola) aliniambia, iliwahi kumtokea (Ernesto) Valverde, niliona mateso ya Luis Enrique."

'Kukosewa hesima'

Aliongeza: "Mara nyingi unahisi kutoheshimiwa , unaona kuwa kazi yako haithaminiwi. Inakuchosha katika suala la afya hasa ya akili, hali yako ya mihemko. Mimi ni mwenye nguvu lakini nguvu hiyo hushuka chini, hadi pale unaposema: haina maana kuendelea.

Barcelona, ​​ambao wamekuwa na matatizo ya kifedha katika misimu ya hivi karibuni, walimteua Xavi kama kocha mnamo Novemba 2021 na alisaidia kubadilisha mwenendo wao, ikiwemo kunyakua taji la ligi msimu uliopita.

Hata hivyo, msimu huu walichapwa mabao 4-1 na Real Madrid katika michuano ya Spanish Super Cup na kutupwa nje ya Kombe la Mfalme na Athletic Bilbao.

"Uamuzi ulinikomboa kwa kiwango binafsi," alisema Xavi, mwezi wa Januari.

'Mabadiliko ya mwenendo'

"Kuanzia Juni 30 sitoendelea kama kocha wa Barca ... kama shabiki wa Barca, nadhani klabu inahitaji mabadiliko ya nguvu."

Tangu Xavi atangaze nia yake ya kuondoka mwishoni mwa msimu kumekuwa na ukosefu wa makocha wenye uzoefu wanaohusishwa na kazi hiyo.

Ni beki wa zamani pekee Rafael Marquez, ambaye kwa sasa anasimamia timu B ya Barcelona, ​​ndiye aliyeonekana kama mbadala halisi wa Xavi.

Kocha wa zamani wa Ujerumani Hansi Flick na Roberto De Zerbi wa Brighton pia walihusishwa na nafasi hiyo.

Licha ya kuwa na msimu usioridhisha, bado Barcelona ina matumaini ya baadaye hasa kwa kuibuka kwa kasi kwa makinda Lamine Yamal, Pau Cubarsi na Fermin Lopez.

AFP