William Ruto

Wakati nchi za Afrika mashariki zikiendelea kukabiliwa na uhaba wa dola, rais wa Kenya William Ruto amejitokeza, akiwaonya wafanyabiashara wanaojilimbikizia dola katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Rais Ruto amezungumza wakati akihutubia Soko la Hisa la Nairobi (NSE) siku ya Jumatano na kusema kuwa serikali yake imeweka mikakati ambayo itahakikisha inamaliza mahitaji ya fedha za kigeni katika siku zijazo.

"Ninatoa ushauri wa bure kwa wale ambao mnakusanya dola, hivi karibuni unaweza kupata hasara. Soko hili litakuwa tofauti katika wiki chache.” amesema Ruto

Benki nyingi za Kenya zilikuwa zikiuza dola kwa kati ya Shilingi 139 na Shilingi 145.50 huku zikinunua kati ya 128.20 na Shilingi 132.5.

"Tumefanya kile ambacho lazima tufanye kama serikali ili kuhakikisha kuwa tunapunguza mzigo kwa watu ambao wanataka kupata faida kwa dola." Rais Ruto alisema.

Ruto alisema mkakati wa utawala wake wa kukabiliana na mzozo huo unalenga kwanza kurejesha soko la kubadilishana fedha baina ya benki ambalo litaona mfumo ambapo benki na taasisi za fedha zinaweza kufanya biashara ya fedha kwa uhuru.

"Ninafuraha kwamba wachezaji katika sekta hii zikiwemo benki zetu wanajitokeza na kufanya kazi na Benki Kuu ili tuweze kusimamia soko letu tena ili kuhakikisha kwamba halijapotoshwa na madalali," alisema Rais Ruto.

Rais aliendelea kusema kuwa hatua hiyo itaiwezesha serikali kupitia utaratibu utakaowezesha waagizaji wa mafuta kununua bidhaa hiyo kwa kutumia shilingi badala ya dola.

Kufuatia onyo la rais, benki kuu ya Kenya (CBK) imetoa agizo kwa benki za humu nchini zenye kanuni mpya ya kubadilisha fedha za kigeni ambayo itaziona benki zikijitathmini mara moja na kuwasilisha kwa benki kuu ripoti ya kiwango chao cha kufuata kanuni mpya kabla ya Aprili 30, 2023.

Uhaba huu katika wiki za hivi karibuni umeshuhudia benki za biashara za Kenya na baadhi ya wafanyabiashara wa Kenya wakipata dola kutoka nchi jirani ya Tanzania na mataifa mengine ya karibu ya Afrika mashariki. Kinachobaki sasa ni kuona soko litapitia nini kwa siku zijazo.

TRT Afrika