Tanzania na Msumbiji wanafungua mpaka wao kwa muda wa saa 12 kil asiku kuwezesha kurejea uhusiano wa kibiashara na kijamii. . Picha : Ikulu Tanzania 

Na Ronald Sonyo

Serikali ya Tanzania imefungua mpaka kati yake na nchi ya Msumbiji baada ya kufungwa kwa miaka 4 kufuatia kuzorota kwa hali ya usalama na kuibuka kwa wimbi la virusi vya Uviko 19.

Mamlaka zimesema zimeridhishwa na hali ya usalama iliyopo hivi sasa, hivyo kufunguliwa kwa mpaka huo kunatoa fursa ya shughuli mbalimbali za kichumi na kijamii kuendelea.

Katika mahojiano na TRT, Mkuu wa Wilaya ya Newala Mkoani Mtwara Alhaj Mwangi Kundya alisema, wasingeweza kufanya lolote kutokana na hali ilivyokuwa awali kwa sababu usalama wa raia ni kipaumbele kwa Serikali.

“Hali ya usalama kwa sasa imeimarishwa katika vijiji ambavyo wananchi wa Msumbiji walikuwa wanaishi na wakahamishwa kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama,'' alisema Mwangi. ''Sasa wananchi wamesharidhia mpaka kufunguliwa kwa sababu hali ya usalama ni shwari, vikosi vya ulinzi vinaendelea na doria kama kawaida na wananchi wanafanya shughuli zao kama ilivyokuwa hapo awali,” Alhaj Mwangi Kundya aliendelea kusema.

Kuhusu biashara ya magendo amesema wamedhibiti hali katika mpaka huo wa Mkunya Kusini mwa nchi na kuwekwa kwa timu ya maafisa wa serikali kama Mamlaka ya Mapato TRA, kikosi maalum cha polisi pamoja na wataalamu wa mazao ili kuangalia kile kinachongia na kutoka ndani ya nchi.

“Kwa ujumla idara zetu zimejipanga vizuri kuhakikisha ukaguzi makini unafanywa ili kutoruhusu mtu yeyote kupita na silaha yeyote iwe kubwa au ndogo, pia tutaimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama,” alisisitiza.

Siku kadhaa baada ya kufunguliwa kwa mpaka huo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dkt Stergomena Tax kabla ya kufunga mkutano wa Tume ya Pamoja ya Masuala ya Ulinzi na Usalama ya tano (JPCDS -5th ) alisema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano kati yake na Msumbiji kwa ajili ya kudumisha amani na usalama kwa raia.

Mkutano huo uliwakutanisha watendaji wa ngazi za juu wa masuala ya ulinzi na usalama kutoka nchi hizo mbili. Jumuiya ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika -SADC iliongeza miezi 12 ya utekelezaji wa misheni yake ili kurejesha usalama wa jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa msumbiji.

Mbali na kuwahifadhi wapigania uhuru na kuongoza mapambano ya uhuru kusini mwa Afrika; nchi hizi zina uhusiano wa kijamii na kiutamaduni. Msumbiji ni miongoni mwa nchi zisizo isahau Tanzania kwa mchango wake wakati wa kupigania uhuru mwaka wake 1975.

Hata hivyo, Septemba mwaka jana, rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alisema kiwango cha biashara kati yake na Msumbiji kimeshuka kutoka shilingi bilioni 53 hadi kufikia shilingi bilioni 26 katika kipindi cha mwaka huo na kuahidi kuongeza uwekezaji pamoja na kulifanyia kazi eneo hilo muhimu.

Kadhia hiyo ya miaka minne imewaathiri watu kutokana na kukosa fursa ya kuingiliana kibiashara na hata ukosefu wa huduma za afya. Hivi sasa wananchi wametakiwa kutumia fursa za kibiashara baada ya ufunguzi wa mpaka huo. Hata hivyo mpaka wa Msumbiji na Tanzania utafunguliwa kwa saa kumi na mbili pekee kila siku.

TRT Afrika