Wanaharakati jijini Nairobi nchini Kenya wameandamana kupinga kupitishwa kwa mswada wa fedha 2023 / Photo: Reuters

Na Coletta Wanjohi

Wanaharakati jijini Nairobi nchini Kenya wameandamana hadi bungeni kupinga kupitishwa kwa mswada wa fedha 2023, ambao serikali ya Rais William Ruto anataka upitishwe.

Mswada huo uliwasilishwa na na serikali bungeni mwezi Mei mwaka huu , ukipendekeza mabadiliko ya ushuru katika sekta tofauti, ambayo yanalenga kupanua wigo wa ushuru na kuongeza mapato ili kukidhi bajeti kuu ya serikali ya zaidi ya dola bilioni 25 kwa mwaka wa 2023/2024.

Je, baadhi ya mambo yapi yanapingwa na wananchi?

  • Kutozwa kwa asilimia 35 ya kiwango cha ushuru kwa watu wenye mapato zaidi ya dola za marekani 3600 kwa mwezi
  • mchango wa asilimia 3 kutolewa na wafanyakazi na waajiri wao kwa ajili ya kufadhili miradi ya nyumba za bei nafuu
  • Kuongezeka kwa ushuru wa mauzo kutoka asilimia 1 hadi asilimia 3
  • ushuru wa asilimia 16 ianze kutozwa kwa maziwa, ambayo yametayarishwa mahsusi kwa watoto wachanga ambayo kwa sasa hayana ushuru
  • Asilimia 15 ya kodi kutozwa kwa mapato yanayopatikana na wanaowekeza katiak kazi za kidijitali
  • Bidhaa za petroli kuongezewa ushuru kutoka asilimia 8 hadi asilimia16

Wananchi wanasemaje?

Mswada huu lazima ipitie bungeni ambapo itapigiwa kura na wabunge.

" Mimi nangojea mbunge mwenye ataenda kupiga kura ati kupinga mpango ya serikali kuwapatia hawa vijana ajira ambao waliwapigia kura , " rais William Ruto alisema Jumapili.

Serikali inatetea mswada huo ikisema itatoa suluhisho ambayo inahitajika kwa kuchochea uchumi, kuunda nafasi za kazi na kuongeza mapato ya wananchi.

Baadhi ya wananchi wanapinga swala la kukatwa mshahara ili kujenga nyumba , wanadai kuwa serikali haifai kumlazimisha mtu kujenga nyumba kwani watu wana mipango tofafuti.

Wengine waliongea katika majadiliano ya mtandaoni ambayo yaliandaliwa na 'Twaweza', shirika linalofanya kazi katika kuwezesha raia kutumia wakala na serikali kuwa wazi zaidi na sikivu nchini Tanzania, Kenya na Uganda.

" Inakaribia kuwa uhalifu kulipwa katika nchi hii, " Nyorude mwananchi aliyechangia majadiliano alisema, " inaonekana kana kwamba hati ya malipo inashambuliwa. Hata sheria hairuhusu waajiri kubadilisha mishahara kwa waajiriwa kwa hasara yao, hivyo unapotaka kutoza ushuru kwenye mapato ambayo tayari yamebanwa matokeo yake ni kuwa unabadilisha mapato ya mfanyakazi kinyume na faida zao."

Wengine wanasema mswada huo utawaumiza wajasiriliamali na vijana.

"Tunaweza kuangalia tasnia ya ubunifu imeajiri vijana wengi sana na vijana hawa baadhi ya vifaa wanavyotumia hata haviko kwenye kiwango lakini bado imewapa fursa ya kuendeleza maudhui yao na kuuza maudhui yao," anasema Purity Jebor, " hivyo unapoanza kuwatoza ada ya ziada itarejeshwa kwa wateja wao na wateja wao hawataweza kuendelea na ada hiyo."

Rais William Ruto anasisitiza kuwa mswada huu ukipitishwa na bunge utawanufaisha Wakenya

Seneta wa kaunti ya Busia Okiya Omtata amewasilisha kesi bungeni kupinga baadhi ya vifungu vya Mswada wa Fedha wa 2023.

Seneta huyo anasema kuwa baadhi ya sehemu zinatishia haki ya kumiliki mali, kupata haki na kukiuka Katiba kwa jumla.

"Nitahusika na haya mahakamani kuhusu maswala ambayo yanatishia kuuwa maendelo ya viwanda na kuturudisha mapangoni. Tututapigania nchi hii mahakamani," Omtata alisema.

Upande wa upinzani umeikashifu serikali ya Rais William Ruto ikidai kuwa analazimisha kupitishwa kwa mswada huu ambao utamfinya mwananchi wa kawaida kiuchumi.

TRT Afrika