Mchekeshaji huyo kutoka Uganda alijizoelea umaarufu kwenye mtandao wa Tiktok mwaka 2021. Picha: Director Edrine 

Na Pauline Odhiambo

Kicheko, mizaha na ucheshi hujulikana kama dawa ya roho, ila kwa Mutaka Abdulrahim Burshir, au Nad kama anavyokulikana na wafuasi wake, kicheko ni dawa ya kuponya ambayo hupunguza huzuni.

Lakini safari ya Mutaka haikuwa ya kupanga. Alikuwa akifanya kazi katika kituo cha kutoa huduma za intaneti wakati wa janga la Covid 19 ndipo wazo la kuunda mtu wa kuchekesha lilipomjia.

Kipindi cha kujifungia kilikatiza masomo yake ya uuguzi, na Mutaka, akiwa na huzuni kwa kumpoteza mjomba wake na babu yake kutokana na ugonjwa wa kisukari.

Mutaka alirekodi video nyingi wakati wa kujifungia ndani, nyingi zikiwa kuhusu changamoto za muziki wa dansi zinazovuma kwenye mitandao ya kijamii.

Kupambana na Sonona

“Nilienea mitandaoni baada ya kufanya zaidi ya video 300 kwenye TikTok lakini kusambaa mitandaoni haikuwa nia yangu kamwe. Nilikuwa nikijitengenezea video hizo kama njia ya kukabiliana na mfadhaiko na kuwaza kupita kiasi,” anaiambia TRT Afrika.

Ilikuwa ni rahisi kiasi kwa Nad kuvaa uhalisia wa uchekeshaji.

Shati na suruali ya kahawia kutoka kwa mjomba wake, pamoja na tai nyeusi ndizo zilizokuwa sare zake. Mavazi hayo yalinakshiwa na koti kubwa na viatu vikubwa kutoka kwa baba yake.

Nad alipata mavazi kutoka kwa baba na mjomba wake./ Picha: Director Edrine

'Kikombe'

Kifaa pekee ambacho hakupewa na mtu ni kikombe chake cha kijani ambacho kimekuwa sehemu muhimu ya uhalisia wake.

"Nilikuwa nikirekodi kipande fulani ndipo nilipohisi kiu. Nilimwomba dada yangu mdogo maji, na ilitokea kwamba akayaleta kwenye kikombe kidogo cha plastiki,” Mutaka anakumbuka.

"Nilikuja kugundua kuwa nimerekodi mchezo mzima nikiwa na kikombe mkononi na niliona tu wakati wa kuhariri ."

Aliipakia video hiyo iliyovutia zaidi ya watazamaji milioni 3 hadi hii leo.

“Mashabiki wangu walifurahishwa sana na kile kikombe, na ndio maana nimeendelea kukitumia na kimekuwa kama alama yangu,” anaeleza.

Nad aliongeza kofia nyeupe na, begi na mfuko wa sokoni kama sehemu ya vifaa vyake.

Aliipakia video hiyo iliyovutia zaidi ya watazamaji milioni 3 hadi hii leo./Picha: Director Edrine

Maudhui yasiyo na mwisho

Mchekeshaji huyo amechapisha zaidi ya video 2,000 kwenye mtandao wa Tiktok na mingineyo ikiwemo YouTube. Video zake huwa na maudhui ya mapenzi na mahusiano ambayo hufurahiwa na mashabiki wake.

"Ikiwa nitafanya mchezo wa kuhuzunisha moyo leo, hata kama haujavunjika moyo leo, najua unaweza kuvunjika moyo kesho, na mchezo huo utakuvutia wakati huo," anasema. "Hili ndilo jambo zuri kuhusu kutengeneza maudhui yasiyo na wakati ambayo hayafi."

Mutaka anasema kuwa baadhi ya ndugu zake walionesha wasiwasi wao kuwa uchekeshaji huo ungeathiri ndoto zake wa kuwa muuguzi, kadiri alivyoendelea kujipatia umaarufu.

“Baadhi ya watu wa jamaa yangu walifikiri kwamba vichekesho vingesitisha masomo yangu ya uuguzi, hivyo wakazungumza na wazazi wangu kuhusu hilo. Lakini nilipowaonyesha wazazi wangu aina ya maudhui niliyokuwa nikitayarisha, waliona ni ya kuchekesha na wamekuwa wakiniunga mkono sana,” asema.

Mmoja wa wajomba zake walikuwa mstari wa mbele kumuunga mkono Mutaka, wakiamini kuwa ipo siku atakuwa maarufu.

Nad amejipatia tuzo kadhaa kupitia uchekeshaji wake./ Picha: Director Edrine

Sifa kimataifa

Mutaka, ambaye ni mhitimu wa cheti cha uuguzi mwaka 2024, amejiunga na kwenye kikundi cha watu maarufu nchini Uganda wanaotumia vipaji vyao kufikia mashabiki wao.

Amefanya kazi na makampuni tofauti ikiwemo ya vinywaji, kitu ambacho kimemfanya kutoka nje ya nchi.

"Watu mara nyingi wananichukulia kama Mwafrika Kusini, Mnigeria au Mkenya, na nadhani hiyo ni kwa sababu ninafanya maudhui yangu katika Kiingereza ambacho kinazungumzwa sana katika nchi kadhaa za Afrika," anasema.

“Takribani asilimia 40 ya mashabiki wangu ni waafrika kusini. Waganda ni asilimia 24.”

Mutaka anafurahia kuchanganya vichekesho na uuguzi.

"Ninafurahia sana uuguzi kwa sababu ninapenda kuwatibu watu, kuwafanya wacheke na kuwaona wakiitikia vyema matibabu," anasema mhitimu wa uuguzi ambaye anajitolea katika hospitali ya serikali nchini Uganda.

Mutaka anaendelea kuhamasishwa na ujuzi kwamba anaweza kuleta furaha na kicheko katika fani zote mbili.

Mchekeshaji Nad./Picha: Director Edrine

Kushinda tuzo

"Nilianza kutengeneza maudhui ya kuweka tabasamu usoni mwangu wakati wa hali yangu ya chini na nikamaliza kuweka tabasamu kwenye nyuso za watu wengine katika mchakato," anasema.

Dhihaka za mitandaoni zilizidi kumwandama lakini hazikumvunja moyo.

"Dhihaka zilikuwa za waziwazi. Baadhi ya maoni yalikuwa mabaya sana kiasi kwamba nilihisi kukata tamaa,” anaiambia TRT Afrika. "Niliamua tu kupuuza maoni hasi kwa sababu nilijua kwamba ikiwa ningezingatia mawazo yangu."

Tangu wakati huo Mutaka ameteuliwa kuwania tuzo nyingi, akishinda taji la ‘Mcheshi Bora’ katika Chanzo cha Tuzo za Nile nchini Uganda 2024 (SONEA) na tuzo nyingine kutoka kwa Waziri Mkuu wa Uganda wa himaya ya mfalme wa Busoga.

Ushauri wake kwa vijana wanaopenda kuunda maudhui: “Kuwa na nidhamu na thabiti. Chagua kitu ambacho unavutiwa nacho na unapenda kufanya na uendelee kukifanya."

Mutaka ameteuliwa kuwania tuzo nyingi, akishinda taji la ‘Mcheshi Bora’ katika Chanzo cha Tuzo za Nile nchini Uganda 2024/ Picha: Director Edrine
TRT Afrika