Ni rahisi kwa wajuzi na wabobezi wa lugha hii kupata kazi sehemu yoyote ile ulimwenguni./Picha: Corona Cermak

Na Corona Cermak

Ajira

Lugha ya Kiswahili ina fursa lukuki katika utoaji ajira.

Kwa mfano, ni rahisi kwa wajuzi na wabobezi wa lugha hii kupata kazi sehemu yoyote ile ulimwenguni.

Ni vyema kwa wadau kuchangamkia fursa hii adimu.

Sanaa za kiswahili kukua na kufika mbali zaidi, muziki, vitabu, filamu utamaduni na michezo. Mfano vitabu vyangu vya watoto ambavyo ni vya kiswahili na kingereza vinapata wanunuzi kwa sababu lugha inakua na inathaminika.

Utamaduni wa waswahili unapata thamani na unatambulika. Hili huvutia watalii kuhamasika kutembelea mataifa yanayozungumza Kiswahili. Watu mbalimbali kutaka kusikiliza nyimbo za Kiswahili na pia kusoma na kutafsiri vitabu vya kiswahili. Wakati mmoja nikiwa matembezini Chekia, nilikutana na vijana wakisikiliza bongo fleva, ilinipa furaha sana.

Kujiamini

Popote ninapokwenda najisikia furaha kuongea kiswahili. Hii ni fursa binafsi ya uhuru wa kuongea na kuisoma lugha yangu mama kama lugha nyingine yoyote.

Hata hivyo, pamoja na fursa hizo za wazi, changamoto nazo si haba.

Changamoto kubwa ni kwamba hakuna walimu wengi wa Kiswahili ambao wanaweza kufundisha Kiswahili kwa kutumia lugha tofauti na kingereza. Walimu wengi wa Kiswahili tunatumia Kingereza kufundisha Kiswahili. Mfano hapa Ulaya mataifa karibu yote yanatumia lugha zao mama. Hivyo hili soko linahitaji walimu wa kiswahili wanaozungumza lugha kama ya kifaransa, Kicheki, Kireno, Kijerumani na kadhalika.

Pili hakuna taasisi ambayo ni kama mwamvuli wa kuhakiki maandiko yote ya Kiswahili. Taasisi itakayotoa mwongozo kwa wadau wote wanatumia kiswahili kama bidhaa. Vipo vitabu vya kufundisha kiswahili vimechapishwa na makampuni makubwa ya lugha lakini ukivisoma vinamakosa chungumzima. Google wanajitahidi ila bado tunahitaji kujaza maneno sahihi kwenye mfumo wao.

Vitabu vya kufundisha kiswahili bado ni vichache mtandaoni. Labda vinapatikana Tanzania lakini nje ya Tanzania bado ni ngumu sana kuvipata. Na wengi wanaojifunza Kiswahili wapo nje ya Tanzania. Vingi ambavyo vipo mtandaoni vimeandikwa na wageni na vina makosa. Niliwahi kukutana na Kamusi ya Kiswahili ambayo imejaa makosa.

Vile vile, baadhi ya walimu wanaojipambanua kujua kufundisha wageni Kiswahili, hawako makini katika namna yao ya ufundishaji. Kwa mfano, hawajua kanuni rahisi za uandishi, wakichanganya R na L au herufi A na H.

Makosa ya namna hii hupotosha wanafunzi, hasa wale wanaojifunza lugha. Pia kuna walimu ambao wanajali maslahi na sio ubora wa kazi, japo wapo wachache wanaopenda kufundisha kwa weledi na uadilifu.

Sisi wenye kiswahili chetu tuna changamoto ya kutopenda kusoma vitabu. Kama hatutasoma, basi hatuwezi kuandika, hivyo tutapata hatari ya kuaandikiwa daima. Kiswahili kitapata Soko zuri kama sisi watumiaji wa kiswahili tutaonyesha bidii kwenye kusoma. Hii itatupa uhakika wa kutoa kazi bora na zenye viwango vya kimataifa.

Pongezi kubwa kwa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), kampuni za uchapishaji kama APE, Mkuki na Nyota na CBO na bila kuwasahahu waandishi wa vitabu vya Kiswahili. Hawa wote wanachangia sana kuleta maendeleo ya lugha ya Kiswahili kupitia kazi zao. Mfano, katika uandishi, uchapishaji au tafsiri za vitabu kwenda lugha ya Kiswahili au Kiswahili kwenda lugha nyingine.

Kiswahili ni lugha yetu, Kiswahili ni nguvu yetu.

Mwandishi wa maoni haya ni mwalimu wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Masaryk cha nchini Chekia.

TRT Afrika