Illustration. Real Madrid hat sich mit Arda Güler (18) von Fenerbahçe Istanbul eines der begehrtesten Talente im europäischen Fußball gesichert. / Photo: AA

Na Nuri Aden

Ni nani chipukizi huyu wa Kituruki anayefananishwa na Lionel Messi?

Msajiliwa mpya wa timu ya Uhispania, Real Madrid, aliyejiunga nao kutoka klabu ya Uturuki ya Fenerbahce, Arda Guler, amekuwa akisakwa na timu mbali mbali kutokana na kipajji chake cha kipekee kilichomuwezesha kuvunja rekodi kadhaa.

Tayari usakataji wake wa soka, umeleta kumbukumbu za Lionel Messi, na kujizolea mamilioni ya mashabiki wanaovutiwa na mpira wake. Mashabiki wa Soka ulimwenguni wamekuwa wakisaka kujua zaidi kuhusu nyota huyo chipukizi aliyezua vita vya usajili kati ya miamba wa Uhispania Real Madrid na Barcelona.

Atakuwa mchezaji ghali zaidi wa Uturuki kusainiwa bara Ulaya, na Mturuki kwanza kuiwakilisha Real madrid tangu Nuri Sahin, aliyekuwepo Santiago Bernabéu msimu wa 2012.

Licha ya kuwa na miaka 18 pekee, ana uzoefu zaidi ambapo ameiwakilisha Fenerbahce mechi 51 na kuvaa jezi ya timu ya taifa ; ‘Milli Takim’ mechi nne. Arda Guler pia anashikilia rekodi ya mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuifungia bao Fenerbahce.

Aidha, Arda ni mchezaji wa tatu mwenye umri mdogo zaidi kuiwakilisha timu ya taifa ya Uturuki alipoingia uwanjani akiwa na umri wa miaka 17, miezi 8 na siku 25 peke kwenye mechi ya hatua ya makundi kufuzu kwa kombe la Ulaya, UEFA EURO 2024.

Arda Guler akiiwakilisha timu ya taifa ya Uturuki. | Picha AA

Arda ni mchezaji mwenye mchanga zaidi kuifungia Uturuki

Mwanasoka huyo, ni mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuifungia Uturuki kufuatia goli lake la guu la kushoto lililomduwaza kipa wa Wales, Danny Ward wiki kadhaa zilizopita akiwa na umri wa miaka 18 na siku 114 pekee.

Arda Guler, mzawa wa Februari 2005 eneo la Altindag, Ankara, nchini Uturuki, alionekana mapema akiwa shule ya msingi, na baadaye kusainiwa na timu ya chipukizi ya klabu ya ligi kuu ya Genclerbirligi alipokuwepo kutoka 2014 hadi 2019.

Mchezaji huyo wa kati, anayetumia guu la kushoto, alisainiwa na klabu maarufu ya Fenerbahçe mnamo Februari 2019 baada ya kung’aa kwenye mashindano ya soka kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 14, na kuhamia jiji kuu la Istanbul kuendeleza safari yake ya soka.

Kwa bahati mbaya, ukuaji wake ulikatizwa ghafla baada ya uviko-19 kukwamisha soka ulimwenguni. Walakin, licha ya hayo, baada ya soka kurejea, Fenerbahce ilimjumuisha kwenye kikosi cha wachezaji wasiozidi miaka 17 na baadaye wasiozidi miaka 19.

Haikumchukua muda mrefu kabla ya kocha wa Fenerbahce kipindi hicho, Vitor Pereira kutambua uwezo wa Arda na kumshirikisha kwenye kikosi.

Arda Güler akiwa mechini kwenye kikosi cha Fenerbahce. Picha | AA

Juhudi za Arda zilimwezesha kusaini mkataba wake wa kwanza mnamo Januari 2021 na kushiriki mechi yake ya kwanza rasmi mwezi Agosti 2021. Miaka miwili tu baadaye, mwezi machi 2022, aliingia mechini kunako dakika ya 74, Fenerbahce ilipokuwa ikichuana na Antalyaspor kwa kuchukua nafasi ya Mesut Özil.

Mnamo mwezi Agosti 2022, alikabidhiwa jezi nambari kumi na rais wa Fenerbahçe Ali Koç kwenye hafla ya kufana mjini Istanbul. Alidhihirisha kuwa alistahili jezi hiyo kwani, mapema mwaka huu, Arda Guler aliorodheswa katika wachezaji 9 chipukizi bora duniani.

Ingawa Uturuki inatajwa kwa kuzalisha nyota wa spoti mbalimbali, wachezaji wake wa soka wanaowakilisha klabu mbalimbali barani Ulaya, ndio wanaozidi kulivutia taifa hilo sifa kemkem kupitia kandanda.

Macho yote sasa yako kwa Arda Guler, kwenye safari yake ya soka barani Ulaya na wengi wanasubiri kwa hamu kuona kipaji chake kikiwasaidia timu yake ya taifa ya Uturuki na vilabu atakavyo viwakilisha hadi atakapostaafu.

TRT Afrika