Wachezaji wa Real Madrid wakisherehekea baada ya ushindi wao wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa UEFA dhidi ya Bayern Munich kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu / Picha: Reuters

Real Madrid walirudi kutoka bao moja chini kwa kujituma kwa "moyo" dhidi ya Bayern Munich na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Jumatano.

Mabao mawili ya Joselu katika dakika ya 88 na 91, zilitosha kuwapatia ushindi wa 2-1 nyumbani na kushinda 4-3 kwa jumla.

Hata hivyo, mabingwa hao wa Uhispania wanasubiriwa na Wajerumani wengine, Borussia Dortmund, katika fainali itakayoandaliwa Wembley, London, Jumamosi, Juni 1.

Itakuwa mara ya kwanza kwa Real Madrid na Borussia Dortmund kukutana katika fainali ya Kombe hilo maarufu la Ulaya.

Madrid walidumisha rekodi yao ya kutopoteza mechi nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa tangu kufungwa 3-2 na Chelsea katika robo fainali ya 2021/22.

Mabingwa hao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara 14, wanalenga taji lao la 15 lakini wanatarajiwa kuwa na kibarua kigumu dhidi ya Dortmund.

Madrid wameshinda fainali 14 kati ya 17 walizocheza.

Kwa upande mwengine, Dortmund ina matumaini ya kushinda kombe hilo kwa mara ya pili, katika kile kitakachokuwa fainali yao ya tatu. Timu hiyo inayoongozwa na Eden Terzić imetinga hadi fainali baada ya kuipiku PSG ya Ufaransa kwenye nusu fainali.

Kufuatia kufungwa na Real Madrid, Bayern imefunga msimu huu bila taji kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2011/12 licha ya nyota wa England wa timu hiyo Harry Kane, kuongoza jedwali la wafungaji akiwa na mabao 11.

Macho yote sasa yapo kwa kocha Carlo Ancelotti wa Madrid, ambaye anafahamu timu za Ujerumani kwani alihudumu katika ligi hiyo kabla ya kufutwa na Bayern Munich mnamo 2017.

AFP