Simba na Yanga katika pechi iliyopita. Timu hizi zinaingia uwanjani leo kutafuta kupenya Ligi ya Mabingwa / Picha : TRT Afrika 

Na Suleiman Jongo

TRT Afrika, Dar Es Salaam, Tanzania

Zinapocheza Simba na Yanga basi shughuli nyingi husimama na mawazo yote huelekea katika mechi zao.

Hii inatokana na ukweli kuwa timu hizi zina mashabiki wengi, zaidi ya nusu au robo tatu ya raia milioni 60 wa Tanzania ni mashabiki wa timu hizi kongwe.

Kila utakayemuuliza basi kama sio shabiki wa Simba, basi atakwambia ni shabiki wa Yanga.

Vivyo hivyo, mashabiki wote wa vilabu hivi vikubwa nchini Tanzania hivi sasa macho na masikio yapo katika mechi zao za mwisho wa wiki.

Yanga, mabingwa wa sasa wa soka nchini Tanzania, wao wakiwa chini ya kocha wao Miguel Gamondi raia wa Argentina, wapo katika maandalizi makali kuhakikisha wanamalizia shughuli katika uwanja wa Chamazi, baada ya mtaji wa magoli 2-0 walioupata katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya ligi ya Mabingwa barani Afrika iliyochezwa wiki mbili zilizopita mjini Kigali, Rwanda.

Na sasa Yanga wanakuwa wenyeji wa mechi hiyo , ikiwa na mtaji mwingine mkubwa wa mashabiki wakiwa uwanja wa nyumbani.

Tayari asilimia kubwa ya tiketi kwa ajili ya mechi hiyo inayochezwa Jumamosi hii zimeshauzwa, huku Yanga ikisisitiza mashabiki kukata tiketi mapema na kufurika katika uwanja wa Chamazi, uliopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

“Tunataka kila mchezaji aje na ufunguo kwa ajili ya kufungua mlango na kuingia hatua ya Makundi,”amesikika Afisa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ally Kamwe akijitapa kuelekea mechi hii.

Amesema Yanga sio klabu kubwa Afrika kwa bahati mbaya, hivyo, wanataka kudhihirisha ubora wao mbele ya wapinzani wao.

Wapinzani wao itabidi kuwa makini na Yanga iliyojaa wachezaji wapiganaji, akiwemo Aziz Ki, mwenye makombora yanayoweza kuleta madhara muda wowote langoni mwa Al-Merreikh.

Pia kiu ya mashabiki wa Yanga ni kumuona kiungo Mahlatse Skudu Makudubela kutoka Afrika ya Kusini endapo kocha atampanga baada ya kurejea katika mazoezi baada ya majeruhi.

Ukiacha mafanikio ya kucheza fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika msimu uliopita, Yanga haijafika katika hatua ya Makundi kwa zaidi ya miongo miwili, hivyo ina chachu hasa ya kufikia tena hatua hiyo katika ligi ya Mabingwa.

Upande mmoja ukitota mwingine wazama

Kwa upande mwingine , wapinzani wao wa jadi Simba nao wana kibarua kigumu cha kugombania mfupa na Power Dynamo ya Zambia baada ya sare ya 2-2 katika mechi ya kwanza walipokuwa ugenini.

Simba, ikiwa chini ya kocha mpya katika msimu huu Roberto Oliviera raia wa Brazil, imedhamiria safari hii kufika japo nusu fainali na kuvuka mstari kabisa hadi fainali ikiwezekana baada ya msimu uliopita kuishia hatua ya Robo Fainali.

Kama ilivyo kwa Yanga, Simba nayo inategemea mtaji wa mashabiki ikiwa uwanja wa nyumbani na imetenga maeneo maalumu yanayojulikana kama ‘Fan Zones’ kwa ajili ya kufunga skrini zitakazokuwa zinaonyesha mtanange huo moja kwa moja (live) kwa mashabiki.

Goli pekee ambalo liliwavusha Simba kwenda hatua ya makundi msimu uliopita lilifungwa na Moses Phiri dhidi ya De Agosto ya Angola katika uwanja wa Benjamin Mpaka jijini Dar es Salaam .

Na ndivyo Simba wanavyoamini tena kuwa historia ya kwenda hatua ya makundi itajirudia tena wakiwa katika ardhi ya nyumbani Tanzania.

Kocha wa Simba amenukuliwa akisema kuwa wachezaji wake wana ari na nguvu ya kuwakabili wapinzani wao tena mbele ya maelfu ya wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo.

Tegemeo kubwa kwa wachezaji wageni

Tofauti na msimu uliopita, kama ilivyo kwa Yanga, Simba pia ina baadhi ya wachezaji wageni wenye jukumu la kuivusha timu hiyo na kuweka historia.

Wachezaji hao ni kama vile Fabrice Ngoma kutoka Al-Hilal na Aubin Kramo kutoka Asec Mimosas.

Lakini pia wanajivunia wachezaji wa kimataifa wengine mbalimbali wenye uzoefu na michuano hii akiwemo Mzambia Clatous Chama, aliyetupia misumari yote miwili katika mechi iliyopoita na Luis Misquissone, aliyerejea tena klabuni hapo akitokea Al Hilal.

Kama ilivyokuwa katika uwanja wao wa nyumbani, Power Dynamo pia wameapa kufa na kupona kuhakikisha wanapata alama tatu na kusonga mbele licha ya Simba kuwa uwanja wa nyumbani.

Haya tusubiri sasa tuone nani atacheka katika dakika 90?

TRT Afrika