Usikilizaji wa kwanza wa kesi iliyowasilishwa na mhudumu wa afya nchini Ujerumani dhidi ya BioNTech kwa madai ya athari za chanjo yake ya COVID-19 utafanyika Jumatatu.
Kesi hiyo iliwasilishwa na kampuni ya uwakili ya Rogert & Ulbrich kwa niaba ya mfanyakazi wa afya wa umri wa makamo.
Mfanyikazi huyo alidai fidia ya €150,000 sawa na dola za kimarekani $161,000 kutokana na madhara ya mwili yanayodaiwa kusababishwa na chanjo hiyo. Anadai kuwa alipata maumivu sehemu ya juu ya mwili, uvimbe kwenye mikono na miguu, uchovu, na matatizo ya usingizi.
Mlalamikaji pia aliomba fidia kwa uharibifu wa nyenzo ambao hauku wekwa wazi.
Rogert & Ulbrich ilitangaza kuwa imewasilisha zaidi ya kesi 200 kwa wateja wanaotaka kulipwa fidia kwa madai ya athari za chanjo.
Pia kuna mashitaka mengine yaliyowasilishwa dhidi ya kampuni hiyo kuhusu suala hilo hilo na Casar-Preller na Caesar-Preller wa Mainz, ambayo ilitangaza kwamba ilifungua kesi takribani 100.
Takriban robo tatu ya dozi milioni 224 za chanjo ya Corona zilizosimamiwa nchini Ujerumani zilitolewa na BioNTech, na madai mengi ya fidia yaliwasilishwa dhidi ya BioNTech, ambayo ilianzisha matumizi ya teknolojia ya mRNA katika chanjo.
Kesi hiyo nchini Ujerumani inawakilisha madai makubwa zaidi ya fidia ambayo BioNTech inakabiliwa nayo ulimwenguni kote tangu kuzuka kwa COVID-19 au Uviko.
Kesi kama hizo zilifunguliwa nchini Italia kwa madai ya athari za chanjo ya chanjo ya Uviko-19 ama Corona kama inavyotajwa na wengi.
Katika taarifa yao iliyonukuliwa na shirika la habari la Anadolu, BioNTech ilisema kwamba baada ya uchunguzi wa kina, ina uhakika kwamba kesi zinazo husika hazikuwa na "msingi" na zitakataliwa.
Ilibainisha kuwa takriban watu bilioni 1.5 duniani kote, ikiwa ni pamoja na takribani watu milioni 64 nchini Ujerumani, wamepewa chanjo hiyo, na hadi sasa, madhara yanayoweza kutokea isipokuwa yale ambayo tayari yameorodheshwa katika maelezo ya bidhaa husika hayaja gunduliwa.