Ukame wapelekea changamoto ya kiafya nchini Somalia

Ukame wapelekea changamoto ya kiafya nchini Somalia

Ukame Afrika Mashariki
Njaa somalia / Photo: Reuters

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, yaani UN FAO, linasema msaada wa kibinadamu sasa unawafikia watu wengi zaidi walioathiriwa na ukame wa muda mrefu nchini Somalia.

"Tuna uwezekano wa kuepusha njaa ya kiwango nchini Somalia," anasema Dk. Chimimba David Phiri, Mratibu wa FAO Afrika Mashariki"

"bado hatujamaliza changamoto hii, inategemea sana na mvua ya msimu wa kuanzia Machi hadi Mei itanyesha kwa kiwango kipi.”

Ripoti Mpya ambayo imezinduliwa na na Wizara ya Afya na huduma za kibinadamu ya shirikisho la Somalia, Shirika la afya duniani na shirika la umoja wa mataifa la watoto yaani UNICEF inasema kuwa inakadiriwa vifo 43,000 zaidi nchini Somalia mwaka 2022 huenda vilisababishwa na athari za ukame wa muda mrefu.

“Tangu mwanzo wa ukame huu, shirika la afya duniani yaani WHO limesema wazi kwamba ukame ni janga la kiafya sawa na janga la chakula na hali ya hewa,” alisema Mwakilishi wa WHO nchini Somalia na Mkuu wa Ujumbe, Dkt. Mamunur Rahman Malik. .

"Tuna matumaini kwamba ikiwa tunaweza kuendeleza jitihada zetu za kujenga sekta ya afya na lishe na mikakati ya huduma za kibinadamu kwa ajili ya kuokoa maisha na kulinda afya za watu walio hatarini, tunaweza kurudisha nyuma hatari ya njaa kabisa," Dkt. Ali Hadji Adam Abubakar waziri wa afya wa Serikali ya Shirikisho la Somalia alisema.

Umoja wa Mataifa unasema misimu mitano mfululizo ya mvua chini ya wastani imesababisha kipindi cha kiangazi ambacho sasa kimewalazimu zaidi ya watu milioni nane na laki tano nchini Somalia kuhitaji msaada wa kuokoa maisha.

Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Mwitikio wa Kibinadamu wa 2023 unatafuta dola bilioni 2.6 kwa ajili ya kukabiliana na janga hiliu nchini Somalia.

TRT Afrika