Picha: Kenya yatangaza kubinafsisha baadhi ya makampuni yake ya serikali / Picha: Reuters

Na Coletta Wanjohi

Kenya inatanguliza masoko ya mitaji kama mradi wa ukuaji wa uchumi.

Uamuzi wa baraza la mawaziri mnamo tarehe 22 mwezi Machi, uliidhinisha mswada mpya wa ubinafsishaji ambao utahusisha mali ya serikali kuuzwa kwa sekta binafsi kupitia masoko ya mitaji ya nchi.

“Tutaorodhesha mali zinazomilikiwa na umma hivi karibuni,” rais William Ruto alisema akiwa katika hafla kwenye soko la hisa la Nairobi, siku ya Jumatano.

Baraza la mawaziri la Kenya limeidhinisha mswada mpya wa Ubinafsishaji ambao utawezesha nchi kubinafsisha baadhi ya mashirika ya serikali.

Mswada huo unapendekeza kwamba hazina ya kitaifa iunde na kuendeleza mpango wa ubinafsishaji wa serikali na kuupitisha kwa baraza la mawaziri ili kuidhinishwa. Mchakato huo hautaomba idhini ya bunge.

Mswada mpya ukiidhinishwa na bunge utachukua nafasi ya sheria ya Ubinafsishaji ya mwaka 2005.

"Sheria iliyokuwepo hapo awali ilifanya iwe vigumu kwa Wakenya kumiliki kipande chochote cha mali ya Kenya," rais alisema, "kukiwa na sheria mpya tunaweza kuweka demokrasia kwa utajiri wetu na kuruhusu mkenya kumiliki kipande cha kile ambacho ni cha nchi yake." William Ruto

Tume ya ubinafsishaji ya Kenya imetaja makampuni 25 zinazolengwa kwa ajili ya ugawaji wa fedha za serikali. Hizi ni pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kenya, Shirika la Agrochemical and Food Corporation, Mamlaka ya Bandari ya Kenya, Kampuni ya Mafuta yani Kenya Pipeline Company na makampuni kadhaa ya sukari.

Baadhi ya wataalam wa sheria, hata hivyo, wamekosoa kipengele cha mswada huo uliolenga kuondoa bunge katika uamuzi kuhusu ubinafsishaji, wakisema kuwa jukumu la bunge la usimamizi katika mchakato wowote ni muhimu.

TRT Afrika