Nchi za Afrika zinataka kuwe na usawa katika mchakato wa kimataifa wa fedha / Photo: AFP / Picha: Reuters

Rais William Ruto ameambia mkutano wa marais unaofanyika Ufaransa kuwa lazima kuwe na usawa katika mchakato wa kifedha wa kimataifa.

" Afrika haitaki chochote cha bure. Lakini tunahitaji mtindo mpya wa kifedha ambapo nguvu haziko mikononi mwa wachache tu," rais Ruto alisema.

Takriban marais 50, kutoka Afrika , wawakilishi kutoka taasisi za fedha za kimataifa, wanachama wa sekta binafsi, wataalam wa hali ya hewa na wanachama wa mashirika ya kiraia wamehudhuria mkutano huu jijini Paris, ulioandaliwa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mnamo Juni 22 na 23.

Rais Ruto alielezea kuwa rasilimali zote hazipaswi kudhibitiwa na benki ya dunia wala Shirika la fedha pekee.

Alisema kusawazisha mchakato wa kifedha kutahakikisha kwamba "sote tunapata rasilimali kwa haki".

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliambia mkutano huo kuwa nchi za Afrika zinakumbwa na changamoto ya madeni na hii inachangia vikubwa wao kutoweza kukabiliana vizuri na athari za tabianchi

" Deni la kibinafsi na la umma limekuwa changamoto kubwa katika nchi nyingi za mapato ya chini," Ahmed amesema. " Siku hizi serikali nyingi zinawaza sana, sio hata kuhusu jinsi ya kuleta maendeleo , ila jinsi tunaweza kulipa madeni."

Wataalamu kadhaa waliohudhuria mkutano huo wamesema kuwa ni lazima kuwe na kiashiria cha mazingira magumu kwa ajili ya kuonyesha wazi ni nchi gani zimeathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi.

TRT Afrika