Jarrad Branthwaite wa Everton akishangilia baada ya kuifungia timu yake bao la kwanza dhidi ya Liverpool./Picha: Getty

Mbio za Liverpool za kutwaa ubingwa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza zimefikia tamati baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa majirani zao wa Everton, kwenye uwanja wa Goodison Park.

Mechi hiyo, iliyobatizwa jina la 'Dabi ya Merseyside', ilishuhudia mchezo mbovu kutoka vijana wa Jurgen Klopp, hasa katika nafasi za ulinzi na ushambuliaji.

Nyota watatu wa Liverpool, Darwin Nunez, Mohamed Salah na Luis Diaz walipoteza nafasi nzuri za kufunga kabla ya kuadhibiwa na Jarrad Branthwaite na Dominic Calvert-Lewin katika vipindi vyote viwili vya mchezo, na hivyo kuipa Everton ushindi wa kwanza wa dabi hiyo katika uwanja wa Goodison toka mwaka 2010.

Kocha Jurgen Klopp wa Liverpool akiomba radhi mashabiki kufuatia kichapo kutoka kwa Everton, Aprili 24./Picha: Getty

Kwa sasa, mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza zimesalia kwa Manchester City na Arsenal, huku vijana wa Pep Guardiola wakiwa na michezo miwili kibindoni.

Mwezi wa Aprili, haukuwa mzuri kwa Klopp hasa baada ya kubanduliwa na Atalanta ya Italia katika michuano ya Ligi ya Ulaya, huku ukiwa ni msimu wa mwisho kwa Klopp ndani ya Anfield.

TRT Afrika