Takriban watu milioni 158 Afrika wanategema punda barani Afrika / Picha kutoka Donkey Sanctuary

Na Coletta Wanjohi

Istanbul, Uturuki

Yule mnyama ambaye unamtegemea kukubea mizigo mizito hapa na pale, hivi sasa amekuwa dhahabu katika soko ya kimataifa.

Huyu ni punda, ambae hivi sasa anasakwa zaidi baada ya mahitaji yake kuongezeka, hasa katika ngozi.

Takriban ngozi milioni 6 ya punda inatumika kila mwaka kutengeneza dawa hiyo ya ejiao. Picha: AFP 

China ndio mtumiaji mkubwa wa ngozi ya punda ambayo inatumika kutengeneza dawa ya kienyeji ya kichina inayoitwa Ejiao.

Dawa hii inatumika katika chakula, vinywaji na bidhaa za urembo. Mahitaji ya ejiao yanazidi kuongezeka katika soko la kimataifa huku sekta ya urembo ikizidi kukua.

Bei yake inasemekana imepanda kwa muongo mmoja kutoka yuan 100 kwa gramu 500 hadi 2,986 ($420).

Lakini kwa nini ukuaji wa mahitaji ya punda kimataifa ni tishio kwa Afrika?

Takwimu zinaonyesha kuwa takriban ngozi milioni 6 ya punda inatumika kila mwaka kutengeneza dawa hiyo ya ejiao.

Ikiwa uzalishaji utaendelea kukua kwa kiwango cha sasa, ngozi zaidi ya milioni 6.8 itahitajika ifikapo 2027. Na hapo China imetegemea punda kutoka Afrika, kutokana na wingi wake wa punda.

Kati ya zaidi ya punda 53 milioni duniani, zaidi ya punda milioni 33 wanasemekana wapo Afrika.

Ethiopia pekee inaongoza kwa zaidi ya punda milioni 9 huku Sudan ikiwa na zaidi ya punda milioni 7.

Chad ina zaidi ya punda milioni 3 huku Niger ikiwa na zaidi ya milioni 2. Kati ya nchi za Afrika Mashariki, Kenya inaongoza kwa punda milioni 1.2.

Mwezi Februari 2024, viongozi wa nchi za Afrika walipitisha uamuzi wa kupiga marufuku uchinjaji wa punda kwa ajili ya ngozi zao katika bara zima.

Hatua hii walisema ni kwa ajili ya kuwatunza punda wa hapa barani ambao wamekuwa wakiuzwa kwa ajili ya ngozi yao.

Taarifa zinaonyesha punda wengine wanaibiwa na hata kuteswa pindi wanaposafirishwa kwenda kwa wanunuzi wao. Takriban watu milioni 158 Afrika wanategema punda.

Tayari nchi kama Uganda, Tanzania, Botswana, Niger, Burkina Faso, Mali, Uganda na Senegal zilikuwa zimepiga marufuku usafirishaji wa punda kwenda China.

Idadi ya punda nchini China imepungua hadi chini ya milioni 2 kutoka milioni 11 mwaka 1992, na kusababisha sekta yake ya e-jiao kutafuta ngozi za punda kutoka mataifa mengine.

Swali ni, je, nchi za Afrika zitaweza kutii marufuku iliyoweka kwa mauzo ya ngozi ya punda kwa soko ya kimataifa?

TRT Afrika