#IXK06 : Kenya under scrutiny amid calls to 'weaken' forest protections / Photo: AFP

Kevin Philips Momanyi

Mke wa Rais wa Kenya, Rachel Ruto atwaa hekta 200 katika Msitu wa Ikweta wa Kakamega, katika jitihada zake za kuimarisha upandajii wa miti nchini kenya.

Siku ya Kimataifa ya Misitu ilipoanzishwa kwa azimio la mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa mnamo Novemba 28, 2013, ilimaanisha upandaji wa miti duniani utaendelea kuimarika.

Kenya kupitia mama Ruto imechagua kuinua bendera hii juu zaidi kwa kuahidi kupanda na kutunza miti milioni 500 ndani ya miaka tisa kabla ya mwaka 2032, ikiwa ni siku moja tu imepita tangu kuadhimishwa kwa Siku ya Kimataifa ya Misitu, inayosherehekewa duniani kote, kila mwaka, Machi 21.

Mama Ruto anafanya kazi bega kwa bega na wake wa magavana 47 kutoka kaunti zote 47 za Kenya kuhakikisha kuwa miti inapandwa na kutunzwa katika kaunti zote hizo.

“Niko hapa Kakamega kutwaa sehemu ya msitu na kupanda miti kuitikia wito wa rais kwamba kufikia 2032, kila Mkenya awe amepanda miti 300. Kama sote tutakubali wito huu, tutakuwa tumepanda miti bilioni 15 katika miaka kumi ijayo,” alisema.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Misitu ni "Misitu na Afya.

Kwamujibu wa Rachael Ruto maeneo wanayoishi watu yakiwa bora,watakua na afya njema na wataishi kwa furaha, hivyo anatoa wito wa jitihada za pamoja ili kuona upandaji wa miti unaongezeka.

“Kama sehemu ya ahadi hii, nimetwaa hekta 200 za Msitu wa Kakamega kwa ajili ya kurejesha misitu. Ninafurahi kufanya kazi na watu binafsi na vikundi vyenye malengo sawa, "alisema.

Haya yanajiri baada Rais William Ruto kudokeza awali kwamba kila Mkenya atakayepanda miti 300 au zaidi atatambuliwa na kutunukiwa cheti; hii ilikuwa katika azma yake ya kuhakikisha kuwa angalau Kenya imepanda miti bilioni 15 kufikia mwaka wa 2032.

Serikali ya Kenya imewataka wanawake wanaoishi karibu na maeneo ya misitu kujilinda dhidi ya uvamizi wa misitu, kutumia nishati safi ya kupikia, na kuepuka matumizi ya kuni na mkaa.

TRT Afrika