Maafisa wa polisi wakabiliana na magenge karibu na Ikulu ya Kitaifa, huko Port-au-Prince, Haiti. /Picha: Reuters

Timu ya maafisa wa polisi wa Kenya, ambao walikuwa wakitathmini kujiandaa kabla ya kikosi cha kimataifa kutumwa kukomesha ghasia nchini Haiti, wanarejea nyumbani baada ya utumaji kazi uliopangwa kuchelewa kutokana na masuala ya kiutendaji.

Timu hiyo inatazamiwa kurejea kutoka Haiti siku ya Jumatatu, baada ya kupendekeza kucheleweshwa kwa kutumwa polisi, hatua ambayo ilitangazwa na rais wa Kenya baadaye.

Afisa mkuu wa Kenya ambaye alikataa kutajwa jina kwavile yeye si msemaji rasmi, alisema vituo hivyo bado vinaendelea kujengwa, na vifaa muhimu zikiwemo magari zinahitajika kabla ya kutumwa kwa maafisa 200 wa kwanza wa polisi kutoka Kenya.

Utumaji wa kikosi hicho ulipaswa kuanza wiki hii, lakini Rais William Ruto alisema utacheleweshwa kwa wiki tatu.

Kituo ambacho polisi watafanya kazi kimekamilika kwa asilimia 70, na kuna haja ya hifadhi ya silaha kuwa salama, kulingana na afisa mkuu, ambaye alikuwa katika timu iliyokwenda mapema kutathmini.

Uthamini wa Marekani

Maafisa hao waliwasili Haiti siku ya Jumanne, walikutana na polisi wa Haiti siku ya Alhamisi, na baraza la mpito la rais siku ya Ijumaa.

Rais wa Marekani Joe Biden, siku ya Alhamisi alitoa shukrani nyingi kwa Ruto, ambaye alikuwa katika ziara ya kiserikali, kwa kukubali kusaidia kukomesha ghasia za magenge nchini Haiti.

Marekani imekubali kuchangia dola milioni 300 kwa kikosi cha kimataifa, kitakachojumuisha maafisa 1,000 wa polisi wa Kenya na wengine kutoka Jamaica, Bahamas, Antigua na Barbuda na mataifa mengine.

Haiti imevumilia umaskini, ukosefu wa utulivu wa kisiasa na majanga ya asili kwa miongo kadhaa.

Uingiliaji kati wa kimataifa nchini Haiti una historia ngumu. Ujumbe wa kuleta utulivu ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa nchini Haiti ambao ulianza Juni 2004, ulikumbwa na kashfa ya unyanyasaji wa kijinsia na kutibuka kwa ugonjwa wa kipindupindu, ambao uliua karibu watu 10,000. Misheni hiyo ilikamilika Oktoba 2017.

TRT Afrika