Nchi zinazoendelea barani Afrika zinataka mgawanyo wa haki wa rasilimali katika kupambana na majanga ya kiafya ya siku zijazo. /Picha: Reuters

Na Sylvia Chebet

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Uelewa wa kuathirika watu kwa pamoja ni jambo muhimu sana. Kuanzia kwa watu wanaopambana na uraibu hadi wale wanaotafuta utulivu baada ya kukumbwa na mikasa, kukiri kuwa katika mazingira magumu mara nyingi ni hatua ya kwanza ya kupoza hisia zilizochemka.

Janga hilo lilikuwa ukumbusho dhahiri kwamba muunganiko wa watu na nchi unavuka mipaka ya kijiografia, na itikadi. Uharibifu uliosababishwa na janga la afya ulimwenguni pia ulithibitisha kuwa usalama wa siku zijazo unategemea ngao ya pamoja iliyoundwa kupitia ushirikiano.

Lakini kama Mkutano wa 77 wa Afya Ulimwenguni uliomalizika huko Geneva ulionyesha, makubaliano hayaji kirahisi.

Baada ya miaka miwili ya mazungumzo kufikia makubaliano ya kimataifa juu ya kushughulikia milipuko ya maradhi ya siku zijazo, rasimu ya mapatano kama haya sasa inaweza kurefushwa kwa sababu ya hali ilivyo sasa ya Geneva.

Mpango huo ulianza 2021, wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipopewa jukumu la kusimamia mazungumzo ya kuamua jinsi ulimwengu unaweza kushiriki vyema rasilimali adimu na kukomesha au kujibu kwa ufanisi milipuko ya siku zijazo.

Tarehe ya mwisho ya kuandaa mkataba wa kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na janga hilo ilikuwa ni Mkutano wa mwisho wa Afya Duniani, ambao ulileta pamoja mawaziri wa afya kutoka nchi 194 wanachama wa WHO.

Hata hivyo, wakati mkutano huo ukihitimishwa, Roland Driece, mwenyekiti mwenza wa bodi ya mazungumzo ya WHO kuhusu makubaliano hayo, alikiri kuwa nchi hazingeweza kukubaliana mara moja kuhusu rasimu.

"Hatuko pale tulipotarajia tulipoanza mchakato huu," alisema, na kuongeza kuwa kukamilisha makubaliano ya kimataifa juu ya kukabiliana na janga ni muhimu kwa ajili ya ubinadamu."

Mwanaharakati wa afya, Maziko Matemba kutoka Malawi, ambaye alihudhuria mkutano huo, alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa na matumaini ya mafanikio.

Malawi, katika Afrika Mashariki, ilikuwa miongoni mwa nchi katika bara hilo zilizobeba mzigo mkubwa wa kuenea kwa Covid-19, kwa sababu ya changamoto kutoka kwa uhaba wa fedha za huduma ya afya hadi uhaba mkubwa wa wafanyakazi wenye uzoefu.

"Mkataba wa kudhibiti majanga, wakati utakapotiwa saini, unapaswa kuonyesha uhalisia wa mambo. Kama hautaandaliwa vyema, madhumuni ya kuwa na makubaliano hayatofanyikiwa," Matemba anaiambia TRT Afrika.

Janga la kiafya limekua ukumbusho dhahiri kwamba muunganiko wa nchi na watu unavuka mipaka ya kijografia, /Picha: AP

Matumaini yenye tahadhari

Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, bado ana matumaini kwamba mkataba utafanyika. Wakati wa hotuba yake katika siku ya mwisho ya mazungumzo, alisisitiza, "Hii sio kushindwa. Tutajaribu kila kitu, tukiamini kwamba chochote kinawezekana, kuhakisha linafanikiwa kwa sababu dunia bado inahitaji mkataba wa kudhibiti majanga."

Precious Matsoso, pia mwenyekiti mwenza wa bodi ya majadiliano ya WHO kwa ajili ya mkataba unaopendekezwa kudhibiti janga hilo, alimuunga mkono Ghebreyesus.

"Tutahakikisha kuwa hii inafanyika kwa sababu wakati janga linalofuata litakapotufikia, hatutapona," alisema.

Rasimu ya awali iliyopendekezwa ya mkataba huo ilijaribu kushughulikia mapengo katika upatikanaji wa chanjo ya Covid-19 kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea.

Hata hivyo, tofauti juu ya usambazaji wa habari kuhusu vijidudu vinavyoibuka na ushirikishwaji wa teknolojia ya kupambana nao iliripotiwa kukwamisha mazungumzo.

Rasimu ya hivi punde inapendekeza WHO kupokea asilimia 20 ya uzalishaji wa bidhaa zinazohusiana na janga kama vile vipimo maalum, matibabu na chanjo. Pia inazitaka nchi kufichua mikataba yao na kampuni za kibinafsi.

Nchi nyingi zinazoendelea zinahisi kuwa sio haki kwamba zinaweza kutarajiwa kutoa sampuli za virusi kusaidia kutengeneza chanjo na matibabu, lakini haziwezi kumudu wakati chanjo hizo zinapotolewa.

Changamoto za ufadhili

Matemba anaona suala la ufadhili ni gumu.

"Pesa hizo zitatoka wapi ni suala inayobishaniwa," anaiambia TRT Afrika.

"Tunawezaje kuhakikisha kuwa kuna pesa zaidi kwa afya, lakini pia afya zaidi kwa pesa?"

Matemba, ambaye alikuwa sehemu ya jopo la hali ya hewa na afya katika mkutano huo, anaamini afya ya umma ndiyo kitovu cha changamoto zote za kimataifa, zinazoathiri Afrika kwa kiasi kikubwa.

"Kwa upande wa Malawi, bado tunapaswa kupata nafuu kutokana na athari za Kimbunga Freddy. Juhudi za misaada zimekatizwa hasa na ukosefu wa fedha," anasema.

Kimbunga Freddy kilitokea Machi 2023 na kudumu kwa siku 36, na kuacha takriban watu 500,000 nchini Malawi wakiwa wameyahama makazi yao na kuharibu mali ya umma na ya kibinafsi yenye thamani ya karibu dola bilioni moja za Kimarekani.

TRT Afrika