Rais wa Marekani, Joe Biden Jumatano alimkaribisha Rais Ruto wa Kenya katika majadiliano kuhusu teknolojia yaliyofanyika Ikulu ya Marekani, Washington, D.C/ Picha kutoka William Ruto 

Rais William Ruto wa Kenya aliwasili jijini Washington, Marekani, Jumatano kwa mkutano na rais wa Marekani Joe Biden.

Akiwa ameambatana na Mke wake Rachel Ruto walilakiwa na mke wa Rais wa Marekani Jill Biden katika ukumbi wa Joint Base Andrews huko Maryland.

Rais wa Marekani, Joe Biden Jumatano alimkaribisha Rais Ruto katika majadiliano kuhusu teknolojia yalifanyika Ikulu ya Marekani, Washington, D.C.

Hii ni siku ya tatu ya ziara rasmi ya rais Ruto nchini Marekani baada ya mualiko wa Rais Biden.

"Ushirikiano wetu ni muhimu, si kwa watu wetu tu bali kwa watu duniani kote. Ikiwa utaendelea kukua jinsi ulivyo nadhani utafaidi sio Marekani na Kenya pekee bali utaongoza na tutakuwa na manufaa duniani kote," Rais Biden alisema.

Marekani na Kenya zinaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano/ Picha kutoka Rais William Ruto 

Rais Ruto aliipongeza U.S. kwa kuweka rasilimali zaidi katika sekta ya kidijitali. Alisema hili litapanua fursa ya ajira na teknolojia barani Afrika.

"Inazungumzia utajiri wa fursa uliopo kati ya Kenya na Marekani. Vijana wetu wenye vipaji, elimu ya ubunifu na teknolojia ya Kimarekani ambayo inapunguza kasi na mtaji wa uwekezaji na wawekezaji ambao wana njaa ya fursa, sio tu nchini Kenya lakini katika bara letu ni fursa inayofaa kwa wakati huu," rais Ruto alisema.

Nchi hizo mbili zinaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano.

Wataalamu wanasema kwa Marekani, ziara hii ni fursa ya kuthibitisha tena uhusiano na mmoja wa washirika wake wa zamani na wanaoaminika zaidi barani Afrika na kuweka upya uhusiano mpana wa kikanda.

Katika Makaburi ya Kitaifa ya Arlington huko Virginia, Marekani, Rais William Ruto alitoa heshima kwa wanajeshi wa Marekani waliokufa / Picha Kutoka Ikulu Kenya.        

Ruto ndiye kiongozi wa kwanza wa taifa la Afrika kufanya ziara ya kiserikali tangu 2008. Kwa Kenya, ziara hiyo inatoa fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano ambao unaweza kufaidi matarajio ya sera ya kigeni ya nchi na uchumi imara unaokua.

Kusaka biashara

Kabla ya kukutana na Rais Biden rais Ruto alitembela jiji la Atlanta ambapo alitoa wito kwa jumuiya ya wafanyabiashara wa Marekani kuwekeza katika fursa mbalimbali za Kenya.

“Kenya iko makini kwa biashara. Tunahimiza wafanyabiashara wa kimataifa kufaidika na uhusiano wa Kenya na Marekani yenye umri wa miaka 60, uhusiano ambao umejikita katika maadili ya pamoja ya demokrasia, uhuru na biashara kuwekeza nchini Kenya,” alisema.

Wakati wa ziara yake katika Makao Makuu ya Kampuni ya vinywaji ya Coca-Cola, kampuni hiyo ilitangaza kuwa itawekeza dola milioni 175, katika kipindi cha miaka mitano ijayo kupanua shughuli zake nchini Kenya.

Rais alizungumza katika Chuo cha Spelman ambapo ushirikiano wa elimu ulitiwa saini ili kuboresha kubadilishana wanafunzi na kitivo, utafiti wa pamoja na uvumbuzi.

Katika Kituo cha Makao Makuu ya Kudhibiti Magonjwa, Rais Ruto alishuhudia utiaji saini wa Makubaliano kati ya kituo cha afya cha Marekani, CDC na Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya, Wizara ya Afya na Mpango wa PEPFAR wa kukumbana na UKIMWI.

kuandaa Mchoro Endelevu wa Mpango wa VVU wa Kenya na tangazo la pamoja la utendajikazi wa Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Umma ya Kenya.

TRT Afrika