Felix Tshisekedi rais wa sasa wa DRC anawania muhula wake wa pili / Picha: AFP

Rais wa Jamhuri ya Kidemokraisa ya Congo Felix Tshisekedi, amesema katika mahojiano kuwa mashariki mwa DRC, watu wengi hawataweza kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Disemba 20 kwa sababu ya hali ya usalama.

Eneo hili limekumbwa na ukosefu wa usalama huku vikundi vyenye silaha vikipambana na jeshi la serikali.

Umoja wa mataifa unasema, tangu Machi 2022, ukosefu wa usalama katika majimbo ya mashariki umefikia kilele kipya, na kusababaisha maafa mengine ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, naukiukwaji wa haki ya kibinadamu.

Takriban wapiga kura milioni 44 waliojiandikisha, kati ya wakazi wapatao milioni 100, watamchagua rais mnamo Desemba 20.

Pia watachagua kati ya makumi ya maelfu ya wagombeaji wa mabaraza ya ubunge na mitaa nchini yenye rasilimali nyingi lakini mizozo na ufisadi uliokithiri.

Eneo la mashariki mwa nchi hiyo limekumbwa na mapigano kwa miongo mitatu, na ghasia zinaongezeka tena baada ya kundi la M23, hivi karibuni kuteka sehemu kubwa ya jimbo la Kivu Kaskazini.

Mapigano hayo yatazuia upigaji kura wa kawaida katika maeneo mawili katika jimbo hilo, lakini mchakato mzima utatishiwa iwapo waasi watauchukua mji mkuu wa jimbo hilo Goma.

Kuongezeka kwa mzozo huo na kuzorota kwa muktadha wa usalama, haswa katika maeneo ya Rutshuru, Masisi, Nyiragongo na Beni kumechangia kuzorota kwa hali ya kibinadamu.

Serikali ya DRC imeeleza rasmi nia yao ya kusitisha ujumbe wa vikosi vya kijeshi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) vilivyowekwa sasa Mashariki mwa nchi hiyo na kuharakisha kuondoka kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa MONUSCO.

"Kwa ujumla, matukio haya yanaibua hofu ya uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa vurugu za kutumia silaha katika wiki au miezi ijayo katika majimbo ya Kivu Kusini, Kivu Kaskazini na Ituri," ofisi ya Umoja wa mataifa ya haki za kibinadamu imesema.

TRT Afrika