Francis Ogolla./Picha: TRT Afrika

Tanzania na Somalia zimetuma salamu zao rambirambi kwa Serikali ya Kenya, kufuatia kifo cha Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo, Francis Ogolla.

Ogolla alikuwa kati ya abiria 11 waliokuwemo ndani ya helikopta hiyo ambayo ilishika moto baada ya ajali hiyo katika eneo la Sindar, kwenye mpaka wa kaunti za Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi, Aprili 18, majira ya saa nane mchana.

Kupitia ukurasa wake wa X, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye yuko nchini Uturuki kwa ziara ya kikazi, alisema kuwa amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kenya, Jenerali Francis Omondi Ogolla na wanajeshi wengine tisa katika ajali ya helikopta iliyotokea katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet, nchini Kenya.

"Natuma salamu za pole kwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Mheshimiwa @WilliamsRuto, wananchi wote wa Kenya, familia, ndugu, jamaa na marafiki wa wote waliopoteza jamaa zao katika katika ajali hiyo. Poleni sana," amesema.

Kwa upande wake, Wizara ya Ulinzi katika Serikali ya Shirikisho la Somalia, imemulezea Jenerali Ogolla kama mtu thabiti aliyesimama imara kwa ajili ya amani ya nchi yake na kanda ya Afrika Mashariki kwa ujumla.

Watu tisa walifariki papo hapo katika ajali hiyo, huku wawili wakijeruhiwa vibaya na kuwahishwa jijini Nairobi kwa matibabu zaidi. Maafisa hao wakuu wa kijeshi, ambao waliondoka katika mji mkuu wa Nairobi siku ya Alhamisi asubuhi, walikuwa kaskazini-magharibi mwa Kenya kwa majukumu ya kiofisi.

Rais Ruto alimteua Ogolla kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi mnamo Aprili 28, 2023, akichukua nafasi ya Robert Kibochi, aliyetimiza umri wa kustaafu.

TRT Afrika