Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (kulia) akipokea shahada ya Udaktari wa Heshima kutoka kwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki Profesa Necdet Unuvar kwenye hafla iliyofanyika Chuoni hapo tarehe 18 Aprili, 2024./Picha: Ikulu ya Tanzania.

Chuo Kikuu cha Ankara cha nchini Uturuki kimemtunuku Rasi Samia Suluhu Hassan wa Tanzania Shahada ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa), katika hafla iliyofanyika chuoni hapo tarehe 18 Aprili, 2024.

Rais Samia amepokea shahada hiyo kutoka kwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ankara, Profesa Necdet Unuvar.

Rais Samia amepokea heshima hiyo kutokana na kuthamini mchango wake kama kutambua jitihada zake kuendeleza mageuzi ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi ambayo yameboresha ustawi wa Watanzania.

"Ni heshima kubwa sana kwangu kutunukiwa shahaha hii na taasisi hii kubwa ya elimu. Naipokea kwa niaba ya Watanzania wote, mimi nabakia kiongozi wao tu nikifanya kila kitu kwa niaba yao," alisema Rais Samia mara baada ya kupokea heshima hiyo.

Kulingana na Rais huyo wa Tanzania, nchi hiyo imeshuhudia ukuaji wa sekta mbali mbali ikiongozwa na ile ya kilimo ambapo uwezo wetu wa uzalishaji wa ndani ulifikia asilimia 124.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Chuo Kikuu cha Ankara tarehe 18 Aprili, 2024./Picha: Ikulu ya Tanzania.

Kulingana na Rais Samia, Tanzania pia imeshuhudia ongezeko la asilimia 5.8 ya mapato kutokana na biashara ya nje ya madini na asilimia 38 ya mapato yatokanayo na Utalii, hizi zikiwa ni baadhi ya sekta zinazochangia pakubwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

"Napokea heshima hii kwa unyenyekevu mkubwa, hasa nikizingatia uvumilivu na ustahimilivu wa Watanzania," aliongeza.

Rais Samia yuko nchini Uturuki kwa ziara ya Kiserikali.

TRT Afrika