Rais Felix Tshisekedi ataiongoza DRC katika muhula wake wa pili. Picha: AFP

Voingozi na wakuu wa nchi mbalimbali wamempongeza rais Félix Tshisekedi kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa mujibu wa matokeo ya Tume Huru ya Uchaguzi DRC, CENI.

Miongoni mwa marais waliompongeza katika ukanda wa Afrika Mashariki ni pamoja na rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, rais wa Kenya William Ruto, rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, na rais wa Uganda Yoweri Museveni.

"Hongera za dhati kwa mheshimiwa Rais Félix Tshisekedi kwa kuchaguliwa tena Kuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ninatarajia kuendelea kufanya kazi pamoja katika kukuza uhusiano kati ya nchi zetu mbili na nchi zetu za Afrika Mashariki," ameandilika rais Samia katika mtandao wa X, zamani Twitter.

"Rais Tshisekedi amechangia vyema juhudi za eneo hili kwa kuileta Kongo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwa kuturuhusu kufanya kazi na jeshi la Kongo katika kukabiliana na ADF Mashariki mwa Kongo," Museveni aliandika kwenye mtandao wa X.

Nae, rais wa Kenya William Ruto alimuandikia ujumbe wa kumpongeza kwenye ukurasa wake rasmi wa X.

"Hongera sana ndugu yangu Mheshimiwa Felix Tshisekedi, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa ushindi uliostahili. Natarajia kuimarisha uhusiano wa Kenya na DRC kwa manufaa ya nchi zetu," ameandika rais Ruto.

Wakati huo huo, rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amempongeza Tshisekedi kwa ushindi kwenye uchaguzi huo akimtaja kama "ndugu na kaka".

Rais huyo wa Burundi Ndayishimiye, ametoa wito kwa upinzani nchini DRC, kutumia njia za kisheria kusaka haki iwapo wanatofautiana na matokeo hayo ya uchaguzi.

Kwa upande wake, rais wa Malawi, Lazarus Chakwera, alisema Malawi inaungana na watu wa DRC kusheherekea hatua hii ya kidemokrasia kwa mchakato wa uchaguzi wa amani.

Rais wa Zimbabwe, Mnangagwa, naye aliandika, "Kwa niaba ya serikali, na watu wa Zimbabwe na kwa niaba yangu, ninampongeza sana Mheshimiwa Félix Antonie Tshisekedi Tshilombo kwa kuchaguliwa tena kwa kura kubwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo."

Kulingana na matokeo hayo, Tshisekedi alifuatwa na mfanyabiashara Moise Katumbi, ambaye alipata asilimia 18 % ya kura, na Martin Fayulu, ambaye alipokea asilimia 5%. Mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel Denis Mukwege, naye alipata chini ya 1%.

TRT Afrika na mashirika ya habari