Viongozi kadhaa wa dini ya Kiislamu pamoja na wanasiasa wamejitokeza kulaamu mashambulizi ya Israel yanayoendelea dhidi ya Palestina. Picha/TRT

Na Gamal Jamil

TRT Afrika, Nairobi, Kenya

Viongozi wa dini ya Kiislamu nchini Kenya wametoa sauti zao za kuunga mkono watu wa Palestina wakati mashambulizi ya Israel yakiendelea Gaza. Hatua hii inakuja licha ya Rais wa Kenya William Samoei Ruto kutangaza kuiunga mkono Israel.

Misikiti kadha nchini Kenya, ikiwemo katika mji mkuu wa nchi hiyo Nairobi leo imetoa Khutba zao za Ijumaa kuonyesha mshikamano na watu wa Gaza huko Palestina.

Akiwa katika Msikiti wa Jamia jijini Nairobi, Sheikh Ibrahim Lethome, ambae ni mjumbe wa Kamati ya Msikiti huo, amelaani shambulio la Wazayuni dhidi ya raia wa Gaza, Palestina na kuwataka Wakenya kusimama na wa Palestina.

“Kwa Waisraeli tunaweza kuwaona ndugu zao (Wamarekani) wanavyowahurumia. Wamarekani walikuwa wa kwanza kusema kwamba watapeleka usaidizi na silaha kwa Waisraeli. Je, sisi tunawahurumia ndugu zetu wa Gaza? Waislamu tuko wapi?” aliuliza.

Aidha amewakosoa maafisa wa serikali walioonyesha mshikamano na Israel akieleza kuwa hawawakilishi jamii ya Kiislamu.

"Waliotoa matamshi ya kuunga mkono Israel na kuwaita watu wa Palestina magaidi hawatuwakilishi. Msimamo wetu ni kwamba watu wa Palestina ni wapigania uhuru wanaopigania ardhi yao, sawa na wapigania uhuru wa Mau Mau waliopigania uhuru wa Kenya,"aliongeza.

Aidha amewataka Waislamu nchini Kenya kufanya dua na kufanya Qunut (dua inayotolewa wakati wa swala katika sehemu maalum wakiwa wamesimama) kwa ajili ya watu wa Gaza.

Katika Msikiti wa Parklands, ulioko katika eneo la Parklands jijini Nairobi, Imamu wa msikiti huo Sheikh Abdurrahman Ishaq alitoa khutbah kuhusu jinsi Palestina ilivyoibiwa na kuwataka waumini hao kuzungumza juu ya dhulma ya Wazayuni.

Zaidi ya hayo, baadhi ya Wabunge wa Kenya walijitokeza kwenye mitandao yao ya kijamii kueleza mshikamano wao na watu wa Palestina.

Miongoni mwao, ni Mbunge kutoka eneo la pwani ya Kenya, Mombasa, Mohammed Ali ambae alichapisha ujumbe uliowagusa Wakenya wengi, akisema, "Viongozi wa Kenya na umma wa Kenya, ambao wana habari kamili kuhusu historia na maendeleo ya mzozo wa Israel na Palestina, simameni na Palestina, na sisi tusiwaonee huruma wakoloni. Nawaombea ndugu zangu wa Kipalestina wapewe uthabiti, subira na nguvu za kujikomboa kutoka mikononi mwa madhalimu."

Vile vile, Mbunge wa Garissa Amina Udgoon Siyad alitumia mitandao ya kijamii kujibu kauli ya Rais Ruto kwamba Kenya itasimama na Israel.

"Mheshimiwa Rais William Ruto, Kenya ni nchi ya kidemokrasia, na tuna mamilioni ya watu wanaofikiri Waisraeli ndio wakandamizaji! Twitter yako haituwakilishi sisi sote kama Wakenya. Mwenyezi Mungu awalinde watu wa #Palestina. magaidi; ni wapigania uhuru," alisema katika akaunti yake ya mitandao ya kijamii

Nae mwanaharakati maarufu wa Kenya Boniface Mwangi, ambaye anajihusisha na harakati za kijamii na kisiasa, alilaani shambulio la Israel dhidi ya watu wa Palestina na kuishutumu serikali ya Marekani kwa kuwasaidia.

"Waziri wa Ulinzi wa Israel aliamuru 'kuzingirwa kamili' kwa Gaza; umeme kukatwa na chakula na mafuta kuzuiwa. Mauaji ya halaiki yameanza. Wapalestina sio Hamas, na kurusha mabomu kwenye nyumba za Wapalestina wasio na hatia ni kuwaadhibu wasio na hatia. Jeshi la Israel linafanya uhalifu wa kivita kimakusudi kwa sababu sugar daddy wao wa Marekani anawalinda.Kuua wanawake, watoto wachanga na vikongwe kwa jina la kulipiza kisasi ni uhalifu wa kivita.Serikali ya Marekani inamsaidia Netanyahu kutekeleza mauaji ya halaiki huko Gaza. Ulimwengu unatazama," alisema kupitia akaunti yake ya mitandao ya kijamii X.

Katika muendelezo wa kuonyesha mshikano na Wapalestina, shughuli maalumu ya kuweka mishumaa siku ya Jumamosi imeandaliwa na mashirika ya Kenya Palestine Solidarity Movement pamoja na Kenya For Palestine.

"Tunafanya mkesha huu ili kuonyesha uungaji mkono wetu kwa watu wa Palestina, ambao wanakabiliwa na mauaji ya halaiki, na kuwaambia watu wa Kenya kusimama na watu wa Palestina," Zahid Rajan, ambae ni Mratibu wa Wakenya kwa Palestina ameiambia TRT Afrika.

Mashirika ya Kiislamu nchini Kenya pia yanapanga mkutano na waandishi wa habari mwishoni mwa juma kulaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza.

TRT Afrika