Air Tanzania (ATCL) yaandaa utaratibu maalumu kwa abiria wake wa safari za Guangzhou

Air Tanzania (ATCL) yaandaa utaratibu maalumu kwa abiria wake wa safari za Guangzhou

Ni miezi mitano tangu Air Tanzania (ATCL) iliporudisha safari zake za China.
Ni miezi mitano tangu Air Tanzania (ATCL) iliporudisha safari zake za China. Picha:Air Tanzania

Shirika la kimataifa la ndege la Tanzania (ATCL) limesimamisha safari zake za moja kwa moja kutoka Tanzania hadi Uwanja wa Kimatifa wa China Guangzhou Baiyun.

Wateja wa shirika hilo wamelazimika kusaka njia mbadala za kufika China ikiwemo kutumia mashirika mengine ya ndege baada ya tangazo la mabadiliko ya ratiba za China kutoka Kampuni ya ndege Tanzania (ATCL).

Kwa mujibu wa mawakala wa safari za ndege, hatua hiyo ni pigo kubwa kwani Air Tanzania ndilo Shirika la kipekee lenye safari za moja kwa moja hadi China.

Matengenezo haya yalipangwa kufanyika kwa awamu lakini kutokana na kuvurugika kwa mfumo wa ugavi (Supply Chain) katika utengenezaji wa vipuri vya ndege uliosababishwa na athari za UVIKO 19; ratiba ya matengenezo ya kawaida kwa ndege zetu zote za Boeing 787-8 (Dreamliner) imepangwa kufanyika kwa pamoja ili kuondoa hatari ya kukosekana kwake kwa muda mrefu ikiwa tutapoteza nafasi ya matengenezo tuliyopangiwa.

Air Tanzania

Kwa upande mwengine, Air Tanzania imechukua hatua hiyo kwa usalama wa abiria wake hata ingawa usitishwaji wa safari hizo, ni hasara kubwa kwa kampuni hiyo.

"Kama tulivyowajulisha abiria wetu, kutakuwa na mabadiliko ya ratiba kutokana na ndege zote mbili (2) za masafa marefu Boeing 787-8 (Dreamliner) kufikia muda wake wa matengenezo ya kawaida (Maintenance Schedule)." Air Tanzania iliandika.

"ATCL itaendelea kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wateja huku ikizingatia usalama wa abiria wake ikiwemo kuhakikisha matengenezo yanafanyika kama ilivyopangwa. Tunaomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza."

Ufafanuzi kutoka kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma ATCL ulisema;

"Huu ni utaratibu wa kawaida kwa mashirika yote ya ndege duniani. Kama ilivyo kawaida, utaratibu maalumu umeandaliwa kwa abiria wote wa safari za Guangzhou, China ili safari zao ziendelee kama kawaida kama walivyofahamishwa hapo awali hadi ndege zitakaporejea."

TRT Afrika