Ethiopia ilipigwa marufuku kutoka kwa AGOA kuanza tarehe 1 Januari 2022. / Photo: AFP

Balozi wa Ethiopia nchini Marekani, Eng. Seleshi Bekele anasema amekutana na uongozi wa Mwakilishi wa Biashara wa Marekani kwa Afrika, huku nchi yake ikiomba kurejea katika mpangilio wa kuingiza bidhaa nchini Marekani bila ushuru, yaani AGOA.

AGOA inaruhusu nchi za Afrika kutuma bidhaa takribani 6500 Marekani . Hizi ni pamoja na nguo, viatu, na bidhaa za kilimo.

"Ni wakati mwafaka wa Ethiopia kurejeshwa kwa manufaa ya AGOA na kusaidia kuongeza uwekezaji," Sileshi alisema kwenye mtandawo wake wa twitter, "tunatumai mkutano unaofuata utawezesha urejeshwaji wetu kwa AGOA."

Ethiopia ilipigwa marufuku kutoka kwa AGOA kuanza tarehe 1 Januari 2022.

Marekani ilisema iliondoa Ethiopia kwa sababu ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu zinazotambulika kimataifa uliofanywa na Serikali ya Ethiopia na vyama vingine huku kukiwa na mzozo unaoongezeka kaskazini mwa Ethiopia."

Ethiopia ilikuwa na vita vya kindani tangu mwaka wa 2020. Serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed na kundi la Tigray People's Liberation Front, walitia saini makubaliano ya amani mnamo Novemba 2022 kumaliza vita.

Kwa nini Ethiopia inataka kurudi AGOA?

Takwimu kutoka kwa mwakilishi wa biashara wa Marekani kwa Afrika zinaonyesha kuwa Marekani iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 572 kutoka Ethiopia mwaka wa 2019. Hili lilikuwa ongezeko la dola milioni 127 kutoka 2018.

Kusitishwa kwa Ethiopia kutoka kwa AGOA kulisababisha baadhi ya makampuni ya kimataifa yaliyokuwa yakizalisha kutoka katika viwanda nchini Ethiopia, kuhamia nchi nyingine kama Kenya na Rwanda.

Mnamo Machi 2023, kampuni inayoitwa Squire Patton Boggs, ikisema inawakilisha Ethiopia iliandika barua kwa Mwakilishi wa Biashara wa Marekani kwa Afrika, kuomba kurejeshwa kwa Ethiopia katika AGOA.

Ilisema kuwa kwa serikali ya Ethiopia na chama cha Tigray People's Liberation Front kutia saini makubaliano ya amani mnamo Novemba 2022 ili kumaliza mzozo kaskazini mwa nchi, nchi hiyo inastahili kurejea katika mtindo huo wa kuuza bidhaa bila ushuru.

Kuondolewa kwa Ethiopia kwa AGOA kumeathiri ajira ya zaidi ya watu 50,000 wengi wao ni wanawake na vijana

Barua hiyo ilisema AGOA imesaidia nchi kubadilisha uchumi wake kuogonza hasa kwa uzalishaji wa sekta ya nguo iliyokuwa inaajiri wanawake wengi.

Kuondolewa kwa Ethiopia kwa AGOA kumeathiri kuajiriwa kwa zaidi ya wananchi 50,000, hasa vijana ambao walifanya kazi katika viwanda vilivyozalisha kwa ajili ya mauzo ya nje.

Ethiopia imesema inatatizika kupata soko jipya la bidhaa kama vile ngozi na bidhaa za ngozi ambazo zilisafirishwa kwenda Marekani kabla ya kusitishwa kwa AGOA.

"Sasa ni wakati mwafaka wa kurejesha ustahiki wa AGOA kwa Ethiopia," anasema Lelise Neme, kamishna wa Tume ya Uwekezaji ya Ethiopia, "itawezesha kuwepo na mzunguko mzuri wa shughuli za kiuchumi, kusaidia kuleta manufaa kwa makampuni ya Marekani, wateja wa Marekani, pamoja na wafanyakazi wa Ethiopia.”

AGOA ilianzishwa mwaka 2000, na baada ya miaka 15 mpango huo ukaongezwa muda hadi 2025. Kwa sasa ni nchi 35 za Afrika kufikia sasa ambazo Marekani imesajiliwa kuwa AGOA.

TRT Afrika