Waandamanaji nje ya Ikulu White House , Washington, wakitaka mashambulio dhidi ya Gaza kusitishwa / Picha: AFP

Ikulu ya White House imefanya karamu ndogo ya futari kusherehekea mwezi mtukufu wa Waislamu wa Ramadhan, huku waalikwa wengi wakisusia wito wa rais kwa sababu ya kukasirishwa kwa jamii ya Waislamu na siasa yake kuhusu vita vya kikatili vya Israel dhidi ya Gaza.

Viongozi kadhaa wa Kiislamu walitarajiwa kuhudhuria mkutano wa Jumanne na Rais wa Marekani Joe Biden, ni Makamu wa Rais Kamala Harris, na maafisa wa serikali ya Kiislamu na viongozi wa usalama wa taifa. Wengine Ikulu ya White House haikuwataja. Baadhi ya watu ambao walikuwa wamehudhuria hafla katika miaka iliyopita, kama vile Meya Abdullah Hammoud wa Dearborn, Michigan, hawakualikwa.

Waislamu wengi, Waarabu na wanaharakati wanaopinga vita wamekerwa na uungaji mkono wa serikali ya Marekani kwa Israel na uvamizi wake wa kijeshi huko Gaza, ambao umesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kusababisha njaa katika eneo dogo la pwani la takriban watu milioni 2.3.

Thaer Ahmad alikuwa miongoni mwa walioalikwa kwenye Ikulu ya White House kwa mkutano uliopunguzwa mwaliko.

"Ilikuwa ni jambo la kushangaza kwamba nilikuwa Mpalestina pekee niliyehudhuria, huku jamii yangu ikiomboleza na kuteseka," Ahmad aliiambia HuffPost. "Nilimwambia rais kwamba nitaondoka. Aliniambia anaelewa kwa nini nilihitaji kuondoka."

Mwaka jana, Biden alikuwa hata hajazungumza neno lolote katika sherehe za Ikulu ya White House ya Ramadhani kabla ya mtu kupiga kelele "tunakupenda." Mamia ya Waislamu walikuwepo kuadhimisha mwisho wa mwezi mtukufu unaofungwa kuanzia macheo hadi machweo.

Hakukuwa na matukio ya furaha kama Ramadhan ya mwaka jana. Wamarekani wengi Waislamu wamekasirishwa na uungaji mkono wa Biden kwa Israel dhidi ya Gaza, Ikulu ya White House ilichagua kuandaa karamu ndogo ya iftar Jumanne jioni. Waliohudhuria walikuwa ni watu wanaofanya kazi katika serikali yake.

"Tunaishi katika ulimwengu tofauti," alisema Wa'el Alzayat, anayeongoza "Emgage", shirika la utetezi la Waislamu. "Ni jambo lisilo la kawaida kabisa. Na inasikitisha."

Alzayat alihudhuria hafla ya mwaka jana, lakini alikataa mwaliko wa kufungua swaumu na Biden mwaka huu, akisema, "Haifai kufanya sherehe kama hii wakati kuna njaa huko Gaza."

Baada ya Alzayat na wengine kukataa mwaliko, alisema Ikulu ya White House ilirekebisha mipango yake siku ya Jumatatu, na kuwaambia viongozi wa jumuiya kuwa ilitaka kuandaa mkutano unaozingatia siasa za serikali. Alzayat bado alikataa, akiamini kwamba siku moja haitoshi kujiandaa kwa fursa ya kugeuza mawazo ya Biden juu ya mzozo huo.

Waandamanaji wakiswali na kuandamana nje Ikulu ya White House, wakitata kusitishwa kwa vita Gaza / Picha: AFP

Kuvunjika Kwa Uhusiano

Kukataa kula - au hata kuwa chumba kimoja - na rais ni ushahidi wazi jinsi uhusiano kati ya Biden na jamii ya Waislamu ulivyovunjika miezi sita baada ya Israeli kuanza vita vyake dhidi ya Gaza.

Rais wa chama cha Democratic alipoingia madarakani miaka mitatu iliyopita, viongozi wengi wa Kiislamu walikuwa na shauku ya kufunga ukurasa wa chuki wa Donald Trump, ikiwa ni pamoja na ahadi yake ya kampeni ya kutekeleza "kufunga na kuzuia kabisa Waislamu kuingia Marekani."

Lakini sasa Wademokrat wanahofia kwamba kupoteza uungwaji mkono kwa Biden na baadhi ya Waislamu kunaweza kusaidia kusafisha njia kwa mpinzani wake wa chama cha Republican kurejea Ikulu ya White House. Uchaguzi wa mwaka huu unaweza kutegemea majimbo machache ya michauno, ikiwa ni pamoja na Michigan yenye idadi kubwa ya Waislamu.

Mohamad Habehh, mkurugenzi wa maendeleo wa Waislamu wa Marekani kwa ajili ya Wapalestina, aliiambia Al Jazeera kwamba Biden hawezi kudai kuwajali Wamarekani Waislamu "kama hatakomesha uungaji mkono wake kwa Israeli."

"Picha hizi wanazofanya - majadiliano haya wanayofanya ili kuonyesha kwamba bado wanaungwa mkono na jumuiya ya Kiislamu - ni majaribio ya kusikitisha ya kujifanya waonekane wazuri wakati ambapo sura zao halisi zimeonekana," Habehh aliiambia Al Jazeera.

Nje ya Ikulu ya White House, wanaharakati walitayarisha futari yao Jumanne jioni katika Hifadhi ya Lafayette. Waandaaji waligawanya tende, tunda la kitamaduni linaloliwa Ramadhan, ili watu waweze kufuturu jua linapozama.

Serikali ya Biden imeendelea kuidhinisha uuzaji wa silaha kwa Israeli, hata kama Waisraeli wakiwaua kiholela Wapalestina na wafanyikazi wa misaada katika Gaza iliyozingirwa.

Nihad Awad, mkurugenzi mtendaji wa Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu, alisema aliwahimiza viongozi wengine wa Kiislamu kukataa mialiko ya kwenda Ikulu ya White House ikiwa wataipokea.

Ujumbe huo, alisema, unapaswa kuwa "isipokuwa atatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, hakutakuwa na mkutano naye au wawakilishi wake."

"Ninaamini kuwa rais ndiye mtu pekee duniani anayeweza kukomesha hili," Awad alisema. "Anaweza kuchukua simu na kumwambia Benjamin Netanyahu, hakuna silaha tena, acha tu mashamblizi, na Benjamin Netanyahu hatakuwa na chaguo ila kufanya hivyo."

TRT World