Wizara ya Afya ya Kenya ilitangaza Jumamosi kuwa imethibitisha maambukizi mapya manne ya ugonjwa wa Ebola, akiwemo ndugu mwingine wa mwathiriwa wa kwanza na wahudumu watatu wa afya waliomhudumia.
Hadi tarehe 6 Oktoba, nchi hiyo haikuwa imeripoti kisa chochote cha virusi hivyo vinavyoambukiza, hadi pale mwanamume Mkenya aliyekuwa akiishi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) alipofariki dunia baada ya kurejea Kenya.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilitangaza mlipuko wake wa 17 wa Ebola mwezi Mei, na tangu wakati huo imeripoti maambukizi zaidi ya 9,000. Ugonjwa huo hatari umesababisha vifo vya watu zaidi ya 15,000 barani Afrika katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.
Katika taarifa yake, Wizara ya Afya ya Kenya "inathibitisha maamvukizi mapya manne ya Ebola", na kufanya jumla kufikia saba, ikiwa ni pamoja na kisa cha kwanza cha mtu aliyefariki dunia.
Hatari kwa umma bado ni 'ndogo'
Wizara ilisema watu hao wanne "walipatwa na homa" na wakatengwa mara moja kabla ya kufanyiwa vipimo, ambavyo vilionyesha matokeo chanya.
"Kesi hizo mpya zinajumuisha ndugu wa karibu wa kiume wa marehemu," ilisema, ikiongeza kuwa mwanamume huyo alikuwa amewekwa karantini tangu tarehe 6 Oktoba.
Wafanyakazi wa afya – wanaume wawili wenye umri wa miaka 29 na 35, na mwanamke mwenye umri wa miaka 32 – walikuwa wamemhudumia mgonjwa wa kwanza, na walikuwa wamewekwa karantini tangu tarehe 9 Oktoba.
Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa "hatari kwa umma kwa ujumla bado ni ndogo," ikisema kuwa "hakuna ushahidi wa maambukizi katika jamii."
Kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa
Kati ya watu 130 waliokutana na wagonjwa, 128 wamepatikana na sasa wako kwenye karantini, iliongeza taarifa hiyo.
Siku ya Ijumaa, wizara ilitangaza kesi ya tatu, mwanamke mwenye umri wa miaka 65 ambaye ni ndugu wa mwathiriwa wa kwanza, na ambaye kwa sasa anapata matibabu. Ndugu mwingine, mwanamume mwenye umri wa miaka 39, pia alikuwa kwenye karantini baada ya kupimwa na kukutwa na virusi hivyo siku mbili zilizopita.
Nchi hiyo haijawahi kuripoti kesi yoyote hapo awali. Nchi jirani ya Uganda ilirekodi watu 20 walioambukizwa—karibu wote wakiwa wamesafiri kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)—na vifo viwili, kabla ya kutangazwa kuwa haina Ebola mwezi Agosti.
Mwathiriwa wa kwanza nchini Kenya hajatajwa jina, lakini alielezewa kama mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 40, ambaye aliugua takriban mwezi mmoja uliopita.
Zaidi ya vifo 4,300 vimerekodiwa nchini DRC
Alikuwa amepata matibabu nchini DRC, kabla ya kusafiri kwa njia ya nchi kavu hadi Kampala, mji mkuu wa Uganda, na kisha kusafiri kwa ndege hadi Nairobi mnamo tarehe 3 Oktoba, ambapo alifariki dunia baada ya kupata matibabu mnamo tarehe 5 Oktoba.
Kulingana na mamlaka za afya za Kongo, mlipuko huo umeambukiza watu 9,066 kufikia sasa na kusababisha vifo 4,381 tangu kuibuka kwa aina ya 'Bundibugyo' ya virusi vya Ebola nchini DRC—aina ambayo bado haina chanjo wala tiba mahususi.























