Wizara ya afya ya Kenya imethibitisha kuwepo kwa mgonjwa wa tatu wa Ebola siku ya Ijumaa wakati akiwa karantini baada ya kutambuliwa kuwa alitangamana na mgonjwa wa kwanza, aliyefariki siku mbili baada ya kuwasili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Wizara ilisema katika taarifa kuwa mgonjwa wa tatu alikuwa mwanamke mwenye umri wa miaka 65 ambaye ni jamaa ya mwanamume wa miaka 40 aliyefariki kutokana na ugonjwa wa Ebola Oktoba 5.
Mwanamke huyo amekuwa karantini tangu Oktoba 6 kwa kuonesha dalili za ugonjwa huo kabla vipimo kuthibitisha.
Mgonjwa wa pili, mwanamume mwenye umri wa miaka 39 kutoka kwenye familia hiyo hiyo, hali yake inaendelea kuimarika, kulingana na Wizara ya Afya.
Maambukizi kwa jamii
Wizara inasema hakuna ushahidi wa ugonjwa huo kusambaa kwa jamii zaidi, kwa kuwa maambukizi yote yanahusishwa na mgonjwa wa kwanza na wote waliotambuliwa wamekuwa karantini.
Ebola inaambukiza kwa haraka na kusambaa miongoni mwa watu waliotangamana, ikiwemo kwenye maeneo ya malazi na nguo.






















