Msanii wa Uganda, aliyegeukia siasa Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine, / Picha: AFP

Msanii Bobi Wine kutoka Uganda amechaguliwa kuwania tuzo za Oscars kupitia filamu yake ya 'Bobi Wine: Rais wa Watu'.

Filamu hiyo, inaelezea changamoto za vurugu wakati wa kampeni ya Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu ya mwaka 2021 alipokuwa akisaka kiti cha nchini Uganda.

"Filamu hiyo ni "simulizi ya mapambano yetu ya uhuru na demokrasia nchini Uganda, kupitia macho yangu na mke wangu, familia yangu na wale ambao ninafanya kazi nao kwa ukaribu", Wine alisema.

Alisema "mwanzoni alisita" kushiriki katika filamu hiyo, ambayo ilioneshwa kwa mara ya kwanza kwenye Tamasha la Filamu la Venice, mnamo 2022.

Hata hivyo baadaye alishawishika na kuwaruhusu watengeneza filamu, Christopher Sharp na Moses Bwayo kumfuata ndani na nje ya njia ya kampeni, wakati alipokuwa akimpinga Rais Yoweri Museveni, ambaye ameongoza Uganda kwa miongo kadhaa.

Ushindi kwenye sherehe za Oscars, mwezi Machi unaweza kuwa "mabadiliko ya hali" kwa Uganda, alisema.

Filamu hiyo ya Bobi Wine, “Bobi Wine: The People’s President” ilikuwa ni moja kati ya filamu 15 zilizovuka hatua ya mchujo kati ya filamu 167 zilizowasilishwa.

"Matumaini yangu ni kwamba dunia itathamini ustahimilivu wa watu wa Uganda, hasa vijana wanaokataa kupoteza tamaa," aliongeza.

Kufikia sasa, filamu hiyo ya Bobi Wine, imepata mafanikio makubwa kwa kutambulika katika tuzo mbalimbali za filamu duniani kote, zikiwemo British Independent Film Awards, Hampton International Film Festival, Independent Film Festival of Boston, Cinema Eye Honours Awards, Docaviv Film Festival, Hollywood Music In Media Awards, One World International Human Rights na Critics Choice Documentary Awards.

Hatma ya filamu hiyo itajulikana Jumapili ya Machi 10, wakati wa hafla ya tuzo makala ya 96 ya Oscars, kulingana na Academy of Motion Picture Arts and Sciences, ambao ndio wenye kuandaa tuzo hizo.

TRT Afrika na mashirika ya habari