Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema kuwa timu ya kukabiliana na hali hiyo ilitumwa haraka baada ya jengo hilo kuporomoka huko Uthiru, Kaunti ya Kiambu mnamo Mei 7, 2024. / Picha: Kenya Red Cross

Watu kadhaa wanahofiwa kukwama ndani ya kifusi baada ya jengo la ghorofa tano kuporomoka karibu na mji mkuu wa Kenya, Nairobi, Jumanne.

Msalaba Mwekundu wa Kenya ulisema katika ukarasa wao wa mtandao wa X, kwamba vikosi vya uokoaji vimepelekwa kwenye eneo hilo.

"Jengo la ghorofa tano limedondoka karibu na Naivasha villas huko Uthiru. Kikosi chetu cha usaidizi kimetumwa," Msalaba Mwekundu wa Kenya ulisema saa 3 usiku kwa saa za Kenya (18:00 GMT).

Uthiru ni kata katika eneo la Kabete katika Kaunti ya Kiambu, kaunti inayopakana na Nairobi.

Hakuna majeruhi au watu waliofariki ambao wameripotiwa hadi sasa.

Mvua kubwa

Sehemu nyingi nchini Kenya zimekuwa zikikumbana na mvua kubwa ambayo imesababisha mafuriko makubwa yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 228, kulingana na takwimu za serikali.

Katika mji wa Nairobi, barabara nyingi zimezibwa kutokana na mafuriko, na nyumba kuzungukwa na maji.

Hata hivyo, mamlaka katika kaunti za Nairobi na Kiambu zimeelezea kuporomoka kwa majengo kunatokana na ubora wa misingi ya ujenzi, ukiukaji wa kanuni za ujenzi, na kuongeza ghorofa zaidi ya miundo ya awali.

Mnamo Novemba 2022, watu watatu walifariki baada ya jengo la ghorofa saba kuporomoka huko Nairobi, huku watu 42 walifariki katika mji mkuu mwaka 2019 baada ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa sita.

TRT Afrika