Vyakula kama mboga na matunda vinaweza kukupa sumu ya kuua usipokuwa makini  / Picha: Getty Images

Na Dayo Yusuf

Wakati shehena ya maziwa ya unga iliyoharibika ilipokamatwa na polisi nchini Kenya, ilisababisha wasiwasi mkubwa na malalamiko nchini Kenya na Mitandaoni.

Wengi walihofia usalama wa afya yao na watoto wao. Hata hivyo hakuna kipya katika hilo maana visa vya vyakula vilivyo haribika kuuzwa Afrika vimezidi.

Lakini kama mtumiaji wa bidhaa, mara ngapi ushawahi kutazama iwapo imepita tarehe ya utumizi kabla ya kununua?

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na chuo kikuu cha Havard umeonesha kuwa ulaji wa chakula kilichopitiliza tarehe yake ya utumizi, unaweza kusababisha kifo cha mapema.

Katika utafiti wao, wanasayansi waliwalisha panya na nzi chakula kilichokaa kabatini kupita muda wake. Matokeo yake yaliwashangaza. Wale wanyama walipungukiwa maisha kwa 10%

Kiukweli wengi wetu hupuuza tarehe hizi katika pakiti hasa ikiwa haikupita pita sana.

Wataalamu wanasema kuwa smaki na nyama zinabeba vimelea hatari zaidi hasa unapoyeyusha kisha ukagandisha tena katika barafu. Picha Reuters

Wataalamu wanasema kuwa ndio, unaweza kubahatisha ukala chakula hicho, lakini inategemea chakula hicho kilihifadhiwa vipi. Wanasema kuwa kugandisha chakula katika barafu kunaweza kusaidia kuhifadhi kwa muda mrefu zaidi ya tarehe ya mwisho iliyopendekezwa kula.

Dkt. Alice Ojwang’ ni mtalamu wa lishe nchini Kenya, na amesema kuwa ni rahisi zaidi kutambua tarehe katika chakula kilicho kwenye mikebe na pakiti.

"Watu wengi hawajui namna ya kutambua chakula kilicho haribika.’’ Ameambia TRT Afrika. ‘ Unaweza kununua vitu kama matunda au mboga na usijue kimepitiliza muda wake, pengine tu kama kimeanza kutoa harufu."

Hili ni tatizo kubwa hasa kwa serikali ambazo zinajikuta katika mchezo wa paka na panya na wauzaji walaghai wanaowapa wateja wao chakula kilicho haribika.

Polisi nhini Kenya wamekamata maguni ya maziwa ya unga yaliyoharibika yaliyokuwa yakinuiwa kuuziwa wananchi Picha : DCI Polisi Kenya  

Mnamo Mei 17, Kenya ilitangaza kuwasimamisha kazi maafisa wakuu 27 wa idara mbali mbali, wakiwemo polisi, kutokana na madai ya kuuza sukari iliyotajwa kuwa hatari kwa afya ya binadamu. Sukari hiyo ililengwa kutumiwa kwa utengenezaji wa kemikali ya ethanol, kwa ajili ya kutumiwa viwandani.

Wataalamu wanasema kuwa visa kama hivi vitaendelea kutokea hasa iwapo kuna watu ambao wako radhi kula chakula hata wakiona ‘vinaota vitu juu yake.’’

Hatari ya sumu ya chakula

Vyakula kama vile nyama na samaki vikiharibika vinaweza kumsababishia mtu sumu mbaya mwilini kutokana na vimelea kama Salmonella, E. coli, H. pylori na niyngine nyingi.

Unaweza pia kujihatarisha kwa vimelea vingine kama vile ukungu, unao ota mara nyingi katika mkate na bidhaa zingine za unga zinapoharibika.

Hii inaweza kukusababishia sumu mbaya sana au kukuzulia maradhi ya mzio, au hata kukuletea maradhi ya muda mrefu kama vile pumu, au maabukizi ya njia za mkojo na vidonda vya tumbo.

Vyakula vingine vinaweza kuota ukungu juu yake ambayo ni hatari sana. mara nyingi vyakula vya unga . Picha AA

Vyakula vilivyo pitiliza muda wake pia havina virutubishi, kumaanisha kuwa utajaza tumbo bila kupata manufaa yoyote kiafya na kukuacha na upungufu wa kinga mwilini kukabiliana na magonjwa.

Dkt. Ojwang’ anatahadharisha pia kuwa wakati mwingine vyakula vilivyogandishwa katika barafu vinaweza kuwa hatari.

"Unaweza kushangaa sana kujua kuwa miongoni mwa vyakula vinavyoweza kukupa sumu ni aiskrimu.’’ Anasema. ‘‘Hatari ipo katika kuyeyusha chakula, kisha kugandisha tena, ambapo unaweka mazingira ya kuota kwa vimelea kama Listeria, ambayo pia hushambulia mboga na matunda zilizogandishwa katika barafu.’’

Miongoni mwa dalili kuwa umepata sumu ya chakula, ni kuumwa na kichwa, homa, kuumwa na tumbo, kuharisha na kutapika. Wataalamu wanapendekeza kutafuta huduma ya matibabu haraka iwezekanavyo kwani baadhi zinaweza kukuua.

Wataalamu wa afya wanashauri kutafuta matibabu ya dharura unapo hisi dalili za kupata sumu ya chakula Picha Getty

WHO inapendekeza siku zote kuchunguza tarehe ya mwishio ya utumizi wa chakula katika pakiti kabla ya kununua.

Ni kawaida kuona wauzaji wakipunguza bei wanapojua chakula kimepitiliza muda wake au kinakaribia, kwa hiyo ni muhimu pia kuwa makini kabla ya kununua.

Dkt Ojwang’ anasema kuwa muhimu zaidi ni siku zote kujua unachokula japo kuna baadhi ya vyakula ambavyo vinakuwa bora vikishakaa.

"Unajua kuwa maziwa yaliyoharibika sio mabaya kunywa. Mwanzo yanakuwa salama sana na nzuri kwa afya. Ilimradi yawe maziwa halisi kutoka kwa mnyama.'' Ameelezea, ''Unaweza kutengeneza maziwa lala, au jabini.’’

TRT Afrika