Sarkodie wa Ghana: Vipi amekuwa mwanamuziki mashuhuri barani Afrika

Sarkodie wa Ghana: Vipi amekuwa mwanamuziki mashuhuri barani Afrika

Rapa kutoka Ghana Sarkodie ni mmoja wa wanamuziki tajiri zaidi barani Afrika, kulingana na Forbes.
Sarkodie, mwanamuziki kutoka Ghana ameshinda tuzo karibia 108 hadi sasa. / Picha: Sarkodie

Na

Brian Okoth

Sarkodie ni mmoja wa wanamuziki maarufu wa kisasa wa Ghana.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 38 ametajwa na baadhi ya mashabiki wake, na hata vyombo vya habari vya burudani, kama rapa mwenye kasi zaidi barani Afrika. Kauli hii, hata hivyo, inaweza kujadiliwa.

Mwanamuziki huyo alizaliwa Julai 10, 1985 katika mji wa Tema, kusini mashariki mwa Ghana. Yeye ni mtoto wa nne katika familia ya watoto watano, jina lake la kuzaliwa ni Michael Owusu Addo.

Sarkodie alipata elimu ya msingi Tema, na baadaye shahada ya kwanza ya usanifu wa michoro kutoka Chuo Kikuu cha IPMC, nchini Ghana.

Safari yake ya kupata umashuhuri

Mtumbuizaji huyo alianza kazi yake ya muziki kama rapa, akishiriki katika mashindano ya kurap yaliyoandaliwa na kituo cha redio cha Ghana.

Ilikuwa wakati wa shindano la rap ambapo alitambulishwa kwa mtayarishaji maarufu wa muziki anayeitwa Hammer of The Last Two.

Hammer alimsaidia Sarkodie kurekodi nyimbo kadhaa, ambazo zilipokelewa vyema na mashabiki wake wa Ghana.

Mnamo Septemba 2009, mwanamuziki wa rapa wa Kimarekani Busta Rhymes alifanya tamasha katika mji mkuu wa Ghana Accra, na Sarkodie alikuwa miongoni mwa wanamuziki wa hapa nchini waliotumbuiza pamoja na msanii huyo wa mgeni.

Sarkodie ni rapa wa kwanaza kutoka Afrika kushinda tuzo la BET. / Picha: Sarkodie

Rapa wa kwanza kutoka Afrika kushinda tuzo ya BET

Mwaka uliofuata, nyimbo za Sarkodie "Push" na "Baby" ziliongoza nchini Ghana.

Albamu yake iitwayo "Rapperholic", ambayo ilitolewa mwaka wa 2012, ilimsaidia Sarkodie kupata uteuzi wake wa kwanza wa BET, na ushindi uliofuata katika kitengo cha "Best International Act".

Hivyo basi, akawa rapper wa kwanza barani Afrika kushinda tuzo ya BET, na pia Mghana wa kwanza kufanya hivyo.

Sarkodie, kwa mara ya pili alishinda tuzo ya BET katika kitengo cha "Best International Flow" Bora mwaka wa 2019. Pia ndiye rapa wa Kiafrika aliyeteuliwa zaidi katika tuzo za BET.

Mazungumzo ya biashara katika shule ya Harvard

Rapa huyo ameshinda tuzo 108 kati ya195 ya mashindano tofauti ya burudani, ikiwa ni pamoja na kunyakua vikombe 28 katika Tuzo za Muziki za Ghana.

"You Go Kill Me", "Adonai" na "No Kissing Baby" ni kati ya nyimbo maarufu za Sarkodie.

Mnamo mwaka wa 2016, rapa huyo alialikwa na Shule ya Biashara ya Harvard, kutoa hotuba kwa wanafunzi kuhusu changamoto wanazo kumbana nazo wanamuziki wa Kiafrika katika kazi zao.

Kimataifa, Sarkodie ameshirikiana na Victoria Kimani wa Kenya; Patoranking wa Nigeria, Runtown na Burna Boy; Diamond Platnumz wa Tanzania; Msanii wa Afrika Kusini marehemu AKA, miongoni mwa wengine.

Ni miongoni mwa wanamuziki matajiri zaidi barani Afrika

Sarkodie mara nyingi anaimba kutumia lahaja yake ya asili ya Twi, ambayo ni sehemu ya lugha za Akan zinazozungumzwa na Waashanti kusini mwa Ghana.

Vyombo kadhaa vya kimataifa, vikiwemo Forbes na The Guardian, vimemweka Sarkodie kama mmoja wa wanamuziki bora na tajiri zaidi barani Afrika.

Kando na muziki, rapa huyo anamiliki biashara ya mitindo iitwayo Sark by Yas, ambayo aliianzisha mwaka wa 2013. Baadhi ya ripoti zimesema anamiliki karibu dola milioni 7 za Kimarekani.

Sarkodie alifunga ndoa na mwenzi wake, Tracy, mnamo Julai 2018. Wana watoto wawili pamoja.

TRT Afrika