Rais wa zamani wa Tanzania Julius Nyerere (Kulia) na mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini Walter Sisulu | Picha: Reuters

Na Matthew Chan-Piu

Uchanganuzi wa historia, jamii, nadharia ya ubinafsi, mapambano, maisha, na utu katika mfumo uliopo wa ubepari ndio msingi wa fikra inayojulikana kama Uafrika Mamboleo - falsafa iliyoundwa na wanazuoni wa Kiafrika katika karne ya 20 kuelezea kuingia na ushiriki wao katika uzoefu mpya wa kihistoria ya sasa.

Hii ilionekana kama njia ya kuunganisha Afrika ya zamani na mpya na kile ambacho wasomi wa Kiafrika walikuwa wamejifunza kuhusu dunia ya magharibi. Kwa mtazamo fulani, fikra hizi zingewapa Waafrika faida za ulimwengu mpya, kuhifadhi urithi wetu, na kutupa mustakabali usiotawaliwa na ukoloni.

Lakini, je, jambo hili limetokea kweli? Je, limefanikiwa? Je, limekuwa la haki?

Wanafalsafa wa hoja hii, kama Natasha Shivji, wanaeleza jinsi ilivyoibuka kutokana na dhana ya muungano wa Kiafrika (Pan-Africanism). "Mjadala wa Pan-Africanism wa miaka ya 1940, 1960, na 1970 ulibeba na kutengeneza wazo la pekee la maana ya kuwa Mwafrika," anasema Dk Shivji, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kisomi wa Historia ya Afrika, jijini Dar es Salaam.

Pan-Africanism ni kanuni au utetezi wa muungano wa kisiasa wa wakazi wote wenye asili ya Afrika. Pan-Africanism ililenga kuilinda Afrika na Waafrika dhidi ya unyonyaji endelevu wa mabeberu waliofanya hivyo kwa karne nyingi.

Kongamano la kwanza la Pan-Africanism lililofanyika Julai 1900 lilikuja na maazimio mbalimbali, ikiwemo waraka yenye kichwa 'Hotuba kwa Mataifa Duniani'. Waraka huo ulitumwa kwa viongozi wa Ulaya, ukitoa wito kwao kukabiliana na ubaguzi wa rangi na kuyapa makoloni katika Afrika na West Indies haki ya kujitawala, haki za kisiasa na nyinginezo kwa Wamarekani wenye asili ya Afrika.

"Mpango huu wa Pan-Africanism, unaeleweka na unaoongozwa na ajenda mahsusi, ulikuwa wa kisiasa na na wenye kupinga ubeberu," Shivji anaongeza. Haukulenga kuingiza na ajenda zingine kama utamaduni. Dhana ya kuwa Mwafrika ana utamaduni wa kipekee haikuzingatiwa sana na viongozi wa kitaifa katika miaka ya 1960 na 1970.

Mbadilishano wa fikra

Wasomi wa Kiafrika walianza kutafiti na kupata uzoefu wa kutoka mataifa ambayo yalionekana kupiga hatua zaidi kimaendeleo: utawala ulikuwa wa haki, uimara wa mfumo wa mahusiano ya kijamii, mifumo ya elimu yenye ufanisi, uhuru wa kujieleza kama haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu, na, muhimu zaidi, mazingira ya kisiasa ambayo yanahimiza watu kuchagua Serikali bora zinawaongoza vyema katika miaka ijayo.

Hakika, lazima hali hii iliwafanya kutamani kuona mengi kama haya yakifanyika nyumbani.

Kwa bahati mbaya, haikuwa hivyo kwa viongozi wengi waliorejea Afrika na kuwakusanya wananchi kutafuta, kudai na hata kupigania uhuru kutoka kwa wakoloni. Fursa ilikuwepo, lakini kwa wengi wa viongozi hawa, ajenda yao ya kweli ingejidhihirisha miaka kadhaa baadaye.

Nimekuwa nikijiuliza kila mara, je, viongozi wetu wakati huo walikuwa na nia ya dhati kutuongoza kwa njia tofauti, au hamasa na miito waliyoitoa mara tu waliporudi nyumbani ilikuwa hila tu?

Mwisho wa yote, walijua kuwa raia wenzao wa nyumbani ambao hawajawahi kukanyaga katika nchi ya wazungu wangesikiliza kwa bashasha yale wanayoahidiwa: nchi ya kufikirika inayotokana na mambo machache yaliyobebwa kwa makusudi kutoka nchi za magharibi kuingizwa ndani ya nchi zao za Kiafrika.

Faida ya kuwa wa kwanza kujifunza kuhusu jambo fulani ni uwezo wa kuhodhi mjadala na miitikio ya wale unaowapelekea habari hio. Wasomi wetu wa Kiafrika walikuwa na fursa ya ziada: wangeweza kuongoza raia kupata uhuru na kuwapinga mabwana wa kikoloni.

Sehemu hii ilikuwa sahihi. Bahati mbaya, wasomi hawa wangeamua na kudhibiti nyakati zinazofuata; kwa sababu, wengi wa raia hawakuwa na elimu au uzoefu wa maisha ambao uliwapa faida ya pekee viongozi wao.

Mugabe Obit

Nisieleweke vibaya: sio viongozi wetu wote wa Kiafrika walikuwa na nia mbaya. Hata hivyo, wengi miongoni mwao walifanya hivyo. Tazama ni nchi ngapi za Kiafrika ambazo hazijakumbwa na dhuluma, ufisadi mkubwa, na misukosuko ya kisiasa.

Ubepari, dhana ya ulafi iliyovikwa vazi la kuvutia?

Shivji anaeleza kuwa haikuwa wazi kabisa mabeberu walikuwa ni akina nani katika miaka ya ’80 na ’90 baada ya ukoloni kushindwa. “Beberu ni nani? Adui wa kikoloni ni nani? Adui wa kweli ni nani?" anahoji mara kadhaa. Hii haihusiani kabisa na kupigana na adui wa kisiasa kwa sababu hatujui adui wa kisiasa ni nani.

Watu walioko madarakani wanafanana kabisa na sisi na wanatumia lugha na mifumo ya kiimani sawa na sisi.

Wanaweza kuwa wanatunyonya. Kwa hakika, watu wanaonyakua ardhi mara nyingi kutoka kwa Waafrika ni Waafrika. Huo ni mfano mmojawapo.

Kama mfumo wa kiuchumi, ubepari umekuwa baraka na laana kwa Afrika. Kwa upande mmoja, ubepari umeleta ukuaji wa uchumi na kuongeza uwekezaji, na kusababisha kuboreshwa kwa miundombinu, upatikanaji bora wa bidhaa na huduma, na hali bora ya maisha.

Tumekuwa na adui mpya, alijeficha ndani, ambaye ametoka mingoni mwetu, wala si kutoka nchi fulani ya mbali. Mabwana wa kikoloni walishindwa, lakini viongozi wetu wapya walidumisha uhusiano na watawala wa kikoloni wa zamani. Na kwa mahusiano hayo, yakawa alama za usaliti.

Mfano ni idadi ya viongozi wapya wa Kiafrika walioibuka na kuanza na kula na kunywa pamoja na wakoloni wa zamani huku wakipewa fedha na uungwaji mkono wa kisiasa ambao ulihakikisha wanadumu madarakani katika nchi zao.

Ubepari una pande nzuri na mbaya na hauko Afrika tu, ni tatizo la dunia. Lakini mifumo yote ya kisiasa na kiuchumi ina faida na hasara zake. Kwa sababu asili ya wanadamu imejikita katika mahitaji na tamaa zao, hakuna mfumo unaoweza kufanya kazi sawia kwa wote.

Mahitaji na matamanio haya ya kibinadamu yaliwasukuma viongozi wetu kuwakandamiza watu wao kimakusudi, na kujenga hofu, chuki na mashaka ili raia wakae kwenye mstari.

Shivji anaweka bayana kuwa kwa sasa haijulikani adui hao ni akina nani. Kwa hivyo, inamaanisha nini kuwa Mwafrika katika hali kama hii? Je, lilikuwa ni wazo la kujiamulia mambo ya kiuchumi au zaidi kutafuta uhuru wa kisiasa, au yote mawili, kwa maneno mengine, kuwa na uhuru wa kiuchumi lakini pia kuwa na uhuru wa kujieleza katika siasa za nchi husika?

Kwa hiyo, kutetea rasilimali zako za kiuchumi ilimaanisha kuzilinda kutokana na ubepari. Hilo halikuwa wazi kwa Waafrika. Je, rasilimali zilikuwepo kwa ajili ya kupata mtaji au kwa jambo la kina zaidi?

Pia ilikuwa ni muhimu kufafanua maana ya Mwafrika - je ni weusi ndio ulikufanya Mwafrika? Je, dini yako ndiyo inakufanya uwe Mwafrika au unachovaa?

Matokeo yake, ubepari huu wa kuogopwa umechochewa na itikadi hii mpya –‘Afrika Inayoinuka’. Dhana hii imependelea wachache ambao wanaweza kufaidika kwa gharama ya watu wengi.

Ulafi huu umekita mizizi katika mfumo wetu wa kimataifa. Binadamu mmoja anatumiwa kwa manufaa ya mtu mwingine.

Kuhusu unyonyaji wa nguvukazi unaotokana na ubepari, Shivji anatoa mfano wa shuka la Wamasai. Shuka ni vazi la Kiafrika lililotumiwa na Wamasai wa Afrika Mashariki. Lakini nguo inapogeuzwa kuwa vazi la mtindo, ni unyonyaji wa kitamaduni, kwani Wamasai hawatapata sehemu ya faida. Tatizo kubwa zaidi ni wakati wale wanaotumia nguo hiyo kama bidhaa hawakubali kama huo ni wizi tamaduni za watu.

Zaidi ya hayo, "hakuna faida yoyote inayonufanisha na kusaidia hali ya Wamasai wanaofukuzwa kutoka kwa makazi yao huko Loliondo kwa faida ya wawindaji wanaotafuta msisimko wa kuua wanyama."

Hili pia ndilo ambalo Uafrika-Mamboleo na Afrika Inainuka zimenuia kufanya, hakuna mpaka tena. Maji yametibuliwa kwa sababu haijulikani nani anamnyonya nani na kwa vile wanyonyaji wapya wa nguvukazi katika nchi zetu pia ni Waafrika wanaodai kuwa kwenye wimbi jipya la Uafrika Mamboleo kwa manufaa ya Waafrika.

Hata hivyo, unyonyaji huu si mpya; ubepari ni mfumo wa kiuchumi unaozingatia misingi ya mali binafsi, ushindani, na kanuni za kubadilishana sokoni. Kutafuta faida na kujipatia mali kupitia shughuli za kiuchumi ni sifa yake kuu.

Hoja ya Afrika Inayoinuka inarejelea wazo kwamba Afrika inafaidika na ukuaji wa uchumi na maendeleo yanayochochewa na ongezeko la uwekezaji, ukuaji wa miji, na utawala bora.

Ubepari ndio kiini cha mjadala wa Afrika Inayoinuka, kwani uwekezaji wa kigeni na biashara za kibinafsi zimechochea ukuaji wa uchumi katika nchi nyingi za Kiafrika.

Hata hivyo, ukuaji huu haujawafikia watu wote, mara nyingi umenufaisha kundi la daraja la kati na juu kiuchumi. Wakosoaji wa ubepari barani Afrika wanasema kuwa umechangia kukosekana kwa usawa wa mapato, uharibifu wa mazingira, na unyonyaji wa wafanyakazi.

Kuna mjadala unaoendelea kuhusu jukumu ambalo ubepari unapaswa kutekeleza katika maendeleo ya baadaye ya Afrika.

Wengine watoa hoja kwamba ubepari ndio ufunguo wa kufungua uwezo wa kiuchumi wa Afrika. Upande wa pili, wengine wanaamini kuwa mfumo mwingine wa endelevu wa kiuchumi unachochoe usawa ndio unahitajika ili kuhakikisha kuwa faida za ukuaji zinafaidisha wengi.

Hatimaye, athari za ubepari kwa Afrika zitategemea sera na taasisi zilizowekwa, pamoja na uwezo wa Serikali za Afrika kudhibiti na kusimamia uchumi wao kwa ufanisi.

Afrika iliyo mbali na ubepari inawezekana tu ikiwa tutaunda mfumo mpya kabisa wa uchumi unaozingatia aina ya uongozi kamili wa kisiasa. Ambayo, kiuhalisia, haitakuwepo kamwe. Kwa sasa, lazima tujaribu na kusimamia sheria na sera zinazotupa nafasi katika mfumo huru na wa haki wa kisiasa na kiuchumi.

Matthew Chan-Piu ni mwandishi na mtengenezaji wa filamu anayepatikana Kampala. Uganda

TRT Afrika