Rais wa Kenya William Ruto ndiye kiongozi wa kwanza wa taifa la Afrika kufanya ziara ya kiserikali Marekani tangu 2008 / Picha: AFP

Na Coletta Wanjohi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Rais wa Kenya William Ruto alifanya ziara rasmi Marekani ya kutoka 20 hadi 24 Mei, 2024 kwa mwaliko wa rais wa Marekani Joe Biden.

Rais Ruto aliambatana na mke wake Rachel Ruto.

Rais William Ruto aliambatanana mke wake Rachel Ruto/ Picha: Rachel Ruto

Ruto ndiye kiongozi wa kwanza wa taifa la Afrika kufanya ziara ya kiserikali tangu 2008, baada ya John Kufuor wa Ghana. Kwa Kenya, ziara hiyo inatoa fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano ambao unaweza kufaidi matarajio ya sera ya kigeni ya nchi na uchumi imara unaokua.

Marekani na Kenya zimekubaliana kujitolea kudumisha haki za binadamu za wote, na kutetea haki zao dhidi ya nguvu za uhuru.

Makubaliano pia yamefanywa katika sekta ya afya, yakilenga kupunguza usambazaji wa ukimwi.

Rais William Ruto alikwenda Marekani na baadhi ya familia yake/ Picha kutoka Rachel Ruto

"Kwa pamoja pia tunathibitisha dhamira yetu ya kukomesha Ukimwi kama tishio kwa afya ya umma nchini Kenya ifikapo 2027, na tunafanya kazi pamoja kutengeneza "Mfumo Endelevu" ili kuunganisha utoaji wa huduma za ukimwi katika huduma za afya ya msingi, kuhakikisha ubora na athari zinabaki,: taarifa ya marais imesema.

Kwa Kenya, ziara ya Rais Ruto inatoa fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano ambao unaweza kufaidi matarajio ya sera ya kigeni ya nchi na uchumi imara unaokua/ Picha kutoka William Ruto

Marekani imewekeza dola bilioni 7 kutoka Mpango wa Dharura wa Rais wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) katika kipindi cha miaka 21 iliyopita.

Zaidi ya hayo, kituo cha taifa cha kuthibiti magonjwa cha Marekani, CDC na Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya zillifanya makubaliano rasmi kuimarisha ushirikiano wao kuhusu uvumbuzi, utafiti na utekelezaji wa sayansi.

Rais wa Kenya William Ruto alitoa maoni yake kuhusu kuwekeza katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa katika Kituo cha Johns Hopkins Bloomberg, Washington, D.C./ Picha kutoka Rais William Ruto

Nchi hizo mbili pia zimekubaliana katika suala la mabadiliko ya tabia nchi.

"Leo tunatangaza kuzinduliwa kwa Ubia kati ya Marekani na Kenya kuhusu Hali ya Hewa na Nishati Safi katika Viwanda ili kuinua hatua za hali ya hewa na ukuzaji wa viwanda wa kijani kibichi kama nguzo muhimu ya uhusiano wetu baina ya nchi hizo mbili," taarifa ya marais hao wawili imesema.

Marekani na Kenya pia zimeahidi kuongeza ushirikiano katika sekta ya nishati safi/ Picha kutoka Rais William Ruto

"Kupitia ushirikiano huu, Marekani na Kenya zinapanga kutanguliza ushirikiano katika maeneo matatu yanayosaidiana ya usambazaji wa nishati safi, misururu ya ugavi wa nishati safi, na ukuzaji wa viwanda wa kijani kibichi," imeongezea.

Marekani na Kenya pia zimeahidi kuongeza ushirikiano katika sekta ya nishati safi na kuendeleza huduma za kupinga mabadiliko ya tabia nchi, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa magari ya umeme na uhamaji, teknolojia ya kukamata kaboni na kuhifadhi, usindikaji wa kilimo cha kijani, teknolojia ya kupikia safi na vituo vya data vya kijani.

Mke wa rais wa Kenya Rachel Ruto akimpa zawadi mke wa Rais wa Marekani Dr. Jill Biden. Picha: Rachel Ruto

Marekani na Kenya zimejitolea kufanya kazi ili kuhitimisha makubaliano ifikapo mwisho wa mwaka kuhusu Ushirikiano wa Biashara na Uwekezaji wa Marekani na Kenya ambao unaakisi malengo na maadili ya pamoja.

"Chini ya mpango huu, serikali zetu zinaazimia kutekeleza ahadi za kiwango cha juu katika maeneo mengi kwa nia ya kuongeza uwekezaji, kukuza ukuaji wa uchumi endelevu na shirikishi, kulinda wafanyakazi, kunufaisha watumiaji na wafanyabiashara, na kusaidia ujumuishaji wa uchumi wa kikanda wa Afrika," Taarifa yao imesema.

Rais wa Kenya William Ruto alikutana na rais wa zamani wa Marekani Barack Obama/ Picha kutoka Rais William Ruto

Nchi izo mbili zimekubali kuendelea kujitolea kwa ushirikiano uliotangazwa hivi majuzi wa kutumia teknolojia ya akili bandia (AI), kuwezesha bila malipo taarifa inayoaminika, na kuharakisha uboreshaji wa ujuzi wa kidijitali.

Kwa kuzingatia mpango huu, serikali za Marekani na Kenya zinakusudia kuanzisha Mazungumzo ya Kimkakati kuhusu akili mnembe AI, ili kujadili kuimarisha maendeleo na usambazaji wa mifumo ya AI iliyo salama na inayoaminika.

Kuhusu amani na usalama, Marekani na Kenya zimekubaliana kuendelea kutoa msaada kwa Somalia, kuiunga mkono serikali ya Somalia katika mapambano yake dhidi ya al-Shabaab, na kuthibitisha tena ushirikiano mkubwa katika mapambano dhidi ya ugaidi na itikadi kali za kivita.

Kenya na Marekani zinasherehekea miaka 60 za uhusiano/ Picha kutoka Rais William Ruto

Viongozi hao wawili pia wamesimama na uamuzi wa Kenya kutuma polisi nchini Haiti, suala ambalo limezua mjadala mkubwa nyumbani.

"Marekani inapanga kutoa zaidi ya dola milioni 300 za usaidizi wa hali ya juu kwa ujumbe hiyo. Kutumwa kwa polisi wa Kenya hadi Haiti, ambapo polisi 1,000 wa Kenya wanalenga kuleta usalama unaohitajika sana kwa watu wa taifa hili la Karibea ni uthibitisho wa kujitolea kwa Kenya, kufikia, na athari ya kimataifa," taarifa ya pamoja ya marais imesema.

Nchi hizo mbili pia zilitangaza ushirikiano mpya wa dola milioni 7 ili kuendeleza na kuimarisha utaalamu wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi ya Kenya, inayolenga zaidi wafanyakazi na maendeleo ya mafunzo.

Nchi hizo mbili zimekubali kuendelea kujitolea kwa ushirikiano uliotangazwa hivi majuzi wa kutumia teknolojia ya akili bandia (AI)/ Picha kutoka Ikulu Marekani

Katika jitihada za kupunguza msongamano katika magereza ya Kenya na kuboresha hali katika vituo vya mahabusu, Washington imetangaza mpango mpya wa dola milioni 2.2 kutoa mafunzo, ushauri na usaidizi wa kiufundi ili kutekeleza mageuzi ya kipaumbele.

Marekani na mashirika yametangaza dola milioni 2.6 (Ksh340.6 milioni) kusaidia mashirika huru ya kiraia. Hii inajumuisha ziada ya $1.3 milioni (Ksh170.3 milioni) ya ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAid) chini ya mpango wa kuwawezesha vijana.

Hii ni kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa kisiasa katika ngazi ya mataifa madogo na $600,000 (Ksh78.6 milioni) ili kuendeleza ushirikishwaji wa walemavu.

Marekani pia inapanga kutumia $700,000 (Ksh91.7 milioni) katika usaidizi mpya ili kuunga mkono juhudi hizi za kuweka msingi, mbinu bora za kimataifa za ulinzi wa mashirika ya kiraia baada ya Rais Ruto kutekeleza sheria ya Shirika la Manufaa ya Umma ya 2013 Mei 9.

Nchi hizo mbili pia zilitangaza ushirikiano mpya wa dola milioni 7 ili kuendeleza na kuimarisha utaalamu wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi ya Kenya / Picha kutoka Ikulu Marekani

Msaada huo ni pamoja na ufadhili wa dola milioni 2.7 (Ksh353.7 milioni) ambao tayari Marekani inatoa ili kuboresha ushiriki wa mashirika ya kiraia katika kusimamia michakato ya utawala.

Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu ya Kenya (Kenha) na Private Equity Everstrong Capital LLC yenye makao yake Marekani wametia saini mkataba wa kuanza ujenzi wa barabara ya mwendokasi ya $3.6 bilioni (Ksh472.9 bilioni) kutoka Mombasa hadi Nairobi.

Marekani pia imepanga dola milioni 250 (Ksh32.75 bilioni) katika uwekezaji mpya nchini Kenya kupitia Shirika la Fedha la Maendeleo ya Kimataifa (DFC), ikijumuisha dola milioni 180 (Ksh23.58 bilioni) kwa mradi mkubwa wa nyumba za bei nafuu. Hilo litaleta jalada la DFC nchini Kenya hadi zaidi ya $1 bilioni (Ksh131 bilioni).

TRT Afrika