Ugonjwa wa Kifua Kikuu huua watu milioni 1.3 kila mwaka. Picha: Wengine

Na Sylvia Chebet

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

"Ndio! Tutaushinda ugonjwa wa Kifua Kikuu!" Hii sio kama kauli mbiu nyengine. Kauli mbiu ya Siku ya Kifua Kikuu inayoadhimishwa tarehe 24 Machi, inaakisi maendeleo ya kisayansi katika kuzuia na kutibu ugonjwa huu barani Afrika.

Kulingana na utafiti wa hivi karibuni uliofanywa Cape Town, Afrika Kusini, dawa zenye nguvu zaidi za kufubaza Virusi Vya Ukimwi huwa na ufanisi zaidi katika kuzuia TB.

Kwa ujumla, matibabu ya kuzuia kifua kikuu au TPT uhusisha dawa moja au zaidi ya kifua kikuu iliyotolewa kwa nia ya kuzuia ukuaji wa ugonjwa wa Kifua Kikuu, linaeleza Shirika la Afya Duniani.

Katika utafiti huo, wataalamu wamegundua ufanisi mkubwa wa tiba ya muda mfupi ya Kifua Kikuu, inayotolewa kila baada ya siku saba, ndani ya kipindi cha wiki 12.

Dkt Ethel Weld, kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Johns Hopkins nchini Marekani anasema kuwa tiba hiyo ya mseto ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Tiba hii huwahakikishia matabibu kuhusu kuanza tiba ya kuzuia Kifua Kikuu mapema kwa watu walio katika hatari kubwa ya ugonjwa wa Kifua Kikuu.

KIla Machi 24, Dunia huadhimisha Siku ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu Duniani./Picha: Wengine

“Tunajua kwamba kuna karibu vifo 200,000 ambavyo vinahusiana na TB kwa watu wenye VVU kila mwaka. Ukweli wa kusikitisha kuhusu hilo ni kwamba kila moja ya vifo hivyo vinaweza kuzuilika,” anasema.

"Kimsingi, matibabu ya mchanganyiko yana uwezo wa kuzuia kesi za Kifua Kikuu na matokeo yote ya kesi za ugonjwa huo ambayo haisababishi kifo tu, bali utegemezi mkubwa kwa wale wanaoachwa pekee," anasema Dkt Weld.

Matokeo haya mapya ni muhimu sana kwa Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambayo ina mzigo mkubwa wa magonjwa hayo mawili.

Kifua Kikuu husababisha vifo milioni 1.3 kila mwaka na huathiri mamilioni ya watu, huku ikiacha athari kubwa za kijamii na kiuchumi.

Mzigo huu huwa mkubwa zaidi kwa mgonjwa, kwani hupambana na hali mbili zenye kutishia maisha.

Huku magonjwa yakihitaji dawa kali ambazo huwaacha wagonjwa wakiwa wamechoka sana, Dkt anasema ilikuwa ni muhimu kupata tiba ya muda mfupi ambayo inaweza kumaliza Kifua Kikuu mapema.

"Wanapoathiriwa zaidi, dawa zinapaswa kuvumiliwa ili wagonjwa wawe na nafasi ya kumaliza matibabu," anasema.

Mzunguko wa Tiba

Ili iwe na ufanisi zaidi, ni vyema dawa hii ikatolewa baada ya mgonjwa kufanyiwa uchunguzi, anaelezea Dkt Weld.

Vimelea vya Kifua Kikuu vipo kila mahali, lakini watu walio na kinga kali hawapati magonjwa. Huwa havina madhara kwa wengine, na kuendeleza kuwa ugonjwa kamili wakati kinga yao inapoathirika, wataalam wanasema.

"Lazima tukumbuke kwamba ikiwa tunaweza kuondokana na maambukizi ya Kifua Kikuu , basi tutaweza kuepuka ugonjwa huu," anasema Dkt Weld.

Tiba hii ni muhimi kukabiliana na Kifua Kikuu. Picha: Wengine

Wataalamu wamependekeza kupitishwa kwa mbinu kukabiliana na Kifuu Kikuu.

"Njia pekee ya kumaliza Kifua Kikuu ni kuzuia viashiria vya magonjwa mapya. Sasa tuna kichocheo cha kufanya hivyo," Gavin Churchyard, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Afya lenye makao yake makuu mjini Johannesburg la Aurum Institute, anaiambia TRT Afrika.

"Kiasi kidogo cha kinga ni uzito mkubwa sana na ni bora kufanya hivyo mapema," anasema.

Jukumu la WHO

Shirika la Afya Duniani limeendelea kuongeza uelewa wa namna sayansi ilivyorahisisha vita dhidi ya Kifua Kikuu.

"Leo, tuna nyenzo, elimu na utashi wa kisiasa ya kumaliza ugonjwa huu ," anasema Mkrugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus

Hata hivyo, kasi ya upatikanaji wa matibabu yake imekuwa sio ya kuridhisha.

Kulingana na Shirika hilo, maendeleo katika kuunda uchunguzi mpya wa Kifua Kikuu, dawa na chanjo bado inakwamishwa na uwekezaji duni katika maeneo haya.

Hii ni licha ya ushahidi kuonyesha kwamba uwekezaji mdogo unaweza kusababisha manufaa makubwa ya kiafya na kiuchumi katika nchi tofauti, na faida ya uwekezaji wa hadi dola 39 kwa kila dola iliyowekezwa.

Wito wa pamoja

Kuzuia maambukizi ni hatua muhimu ya kumaliza Kifua Kikuu.

Ili kutekeleza hilo, ni muhimu kutoa matibabu ya kuzuia Kifua Kikuu kwa watu walio katika hatari kubwa.

"Unyanyapaa hutokana na ukweli kwamba mara tu unapopata ugonjwa huu, mtu anaweza kuusambaza kwa wapendwa wake," anaeleza Dk Weld.

"Lakini dawa hii ya mseto inatoa kinga kubwa kwa familia na watu wenye umri mkubwa."

Dkt Tereza Kasaeva, Mkurugenzi wa Mpango wa Kifua Kikuu ndani ya WHO, anasema kuwa Shirika hilo litaendelea kutoa uongozi wa kimataifa katika kupambana na Kifua Kikuu.

"WHO itaendelea fanya kazi na wadau wote katika kuokoa watu, familia na jamii iliyoathiriwa na ugonjwa huu hatari."

TRT Afrika