Zaidi ya wilaya 30 zimekumbwa na ugonjwa wa mifugo wa miguu na midomo/ Picha kutoka Janet Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameiomba Misri kutengeneza chanjo nyingi zaidi za mifugo dhidi ya ugonjwa wa miguu na midomo yaani 'Foot and Mouth disease,' FMD.

"Munapaswa kutengeneza chanjo zaidi, kwa sababu Uganda ina mifugo mingi. Uganda ina mifugo milioni 44,” Rais Museveni aliiomba serikali ya Misri.

Rais Museveni alikuwa akikutana na ujumbe wa serikali ya Misri katika shamba lake la Kisozi Wilayani Gomba.

Zaidi ya wilaya 30 zimekumbwa na ugonjwa wa miguu na midomo ukihatarisha maisha ya wanyanya na afya ya wananchi hasa kwa nyama inayouzwa.

Ugonjwa wa miguu na midomo (FMD) ni ugonjwa mbaya, unaoambukiza sana wa mifugo. Ugonjwa huu huathiri ng'ombe, nguruwe, kondoo, mbuzi na wanyama wengine wa kucheua wenye kwato. Wanyama wanaofugwa wanaathirika sana.

Misri imeiuzia Uganda chanjo milioni 10 kwa dola senti 0.9 kwa kila dozi.

Tayari dozi milioni 3 zimewasili na hii, Wizara ya Kilimo inasema itaongezewa kwa dozi 900,000 ambazo tayari zimesambazwa katika wilaya 46.

Rais Museveni alisema mbali na ng’ombe milioni 16, wapo mbuzi, nguruwe, miongoni mwa mifugo wengine ambao wanajumuisha idadi ya mifugo nchini kufikia milioni 44 na wote wanahitaji kuchanjwa.

Serikali imepanga kuunda hazina ili kuirahisishia kuanza ununuzi wa chanjo ya FMD kwa wanyama wote milioni 44.

Wakulima pia wamearifiwa kuwa watalazimika kuzingatia chanjo ya kila mwaka ya FMD na uthibitisho wa chanjo utakuwa sharti la awali la biashara ya wanyama na/au bidhaa za wanyama.

FMD hupatikana kupitia njia ya mate, wanapopumua na hata kinyesi cha wanyama walioambukizwa. Wanyama wengine kupitia njia ya kupumua au ya mdomo. Virusi vinaweza kuwepo kwenye maziwa kwa muda wa siku 4 kabla ya mnyama kuonyesha dalili za ugonjwa.

Serikali ya Uganda inasema kwa wanyama wake milioni 44 inahitaji dozi milioni 88 kuendesha zoezi hilo kila mwaka.

Kulingana na Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo zaidi ya dola milioni 176 itahitajika kwa kazi hiyo kwani kila dozi inagharimu $2.

TRT Afrika