A general view of the Diamond Cement factory facilities in Mindouli in the war-torn region of Pool, south of Congo-Brazzaville, is seen on July 23, 2019. / Photo: AFP

Kambale Makolongo, mfanyabiashara wa Kongo, alisema amejisikia faraja baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikiwa ni mwanachama wa saba.

Mnamo mwaka 2019, DRC iliomba uanachama kwa matumaini ya kuboresha uhusiano wa kibiashara na kisiasa na majirani zake wa Afrika Mashariki hasa hasa Kenya na Tanzania.

Mwezi Machi 2022, uanachama huo uliidhinishwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo ilimaanisha kuwa watu milioni 90 nchini DRC wangeweza kutembea kwa uhuru na kufanya biashara katika nchi zingine sita za Afrika.

Ilimaanisha pia biashara itakuwa ya haraka, rahisi na ya bei nafuu kwani uanachama ulimaanisha kuwa ingepanua kwa kiasi kikubwa eneo la kambi ya biashara.

Lakini mwaka mmoja baadae, bado analipa $45 kwa ajili ya kupima Uviko-19 na $50 kwa visa ya miezi mitatu ya kuingia nchi ya jirani ya Uganda.

"Ninafanya safari tatu au nne kati ya DRC na Uganda ambazo zilinigharimu takriban dola 300 kwa malipo ya viza - kama viza ni bure kwa ajili yetu, dola hizo 300 zinaweza kunisaidia kufanya mambo mengine," Makolongo aliiambia TRT Afrika.

Kulingana na vyanzo rasmi ndani ya EAC, sheria na kanuni za EAC bado zinahitaji kuidhinishwa na wabunge nchini Kongo kabla ya kuanza kutumika.

Kutokana na hali hiyo, raia wa DRC wanaotaka kusafiri kwenda nchi nyingine bila viza wanaweza kusubiri kwa muda hadi mchakato wa makubaliano uishe, ambao unaweza kuchukua miezi kadhaa au hadi mwaka moja.

Mchakato kama huo ulichukua miezi minne kwa Sudan ya Kusini kuwa mwanachama kamili wa EAC baada ya kuafiki mkataba wa jumuiya mwezi Aprili 2016.

Mfanyabiashara mwingine, Maguy Mundeke, alisema madereva wengi wanaokuja Uganda, Kenya na Tanzania wanakabiliwa na matatizo kadhaa, kama vile kupanga foleni kwa ajili ya kupata viza ya kuingia DRC, kusubiri siku kadhaa ili bidhaa zao ziondolewe mpakani, na kupata maegesho makubwa pamoja na gharama za kuegesha lori.

"Bidhaa zangu zinakaa siku kadhaa mpakani zikisubiri kibali, hivyo kama tungekuwa tayari kuvuka, inaweza kuwa rahisi sana kwangu lakini pia kupunguza gharama za uuzaji wa bidhaa zangu nchini DRC," Mundeke aliiambia TRT Afrika.

Wakongo wengi waliohojiwa na TRT Afrika pia wanatumai kuona Jumuiya ya Mataifa ya Afrika Mashariki ikiikubali lugha ya Kifaransa kama lugha ya jumuiya hiyo ili kurahisisha kwa wazungumzaji wa Kifaransa nchini DRC kujumuika.

Kuunganisha nchi kubwa na yenye machafuko kama DRC katika maeneo mengine ya EAC ni kazi ngumu.

Miundombinu duni na hali ya usalama nchini inatia mashaka hasa mataifa ya EAC.

Kulingana na wataalam wa biashaŕa, miundombinu katika vituo vya mpakani vinavyoingia DRC haitoshi na ni hafifu ikilinganishwa na ile ya nchi nyingine.

Barabara zinazoelekea katika miji mikubwa nchini DRC pia zinahitaji ukarabati mkubwa, kwani barabara ziko katika hali mbaya sana.

Zaidi ya hayo, kuna wasiwasi kuhusu ukosefu wa usalama nchini.

Akihojiwa na TRT Afrika, Profesa Solomon Asimwe, mchambuzi wa masuala ya usalama na siasa barani Afrika, alisema nchi za Afrika Mashariki zinatumia vitambulisho vipya na vya kisasa zaidi katika kuvuka mipaka ambayo DRC bado haijatekeleza, hivyo wakongo bado watalazimika kusubiri kabla ya kuruhusiwa kusafiri bila kulipa ada ya visa.

"Hofu yangu ni kwamba mataifa mengine yanaogopa hali ya usalama nchini DRC kwa sababu bado kuna ukosefu wa utulivu," Profesa Asimwe aliiambia TRT Afrika.

"Kwa maoni yangu, kujiunga kwa DRC katika Mataifa ya Afrika Mashariki ni suala lililoharakishwa kwa sababu DRC lazima kwanza ishughulikie baadhi ya matatizo ya ndani kama vile ukosefu wa usalama, uhuru wa kujieleza, rushwa na demokrasia."

TRT Afrika